VIDEO: Mwakyembe: Uchaguzi Yanga pale, TFF kusimamia

Muktasari:

  • Nafasi zinazojazwa kwenye uchaguzi huo ni ile ya Mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji.

Dar es Salaam. Ile filamu ya uchaguzi wa klabu ya Yanga imefikia tamati baada ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutoa msimamo wa Serikali kuwa uchaguzi huo utafanyika pale na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Dk Mwakyembe Leo Jumatatu alimaliza mzizi wa fitina katika kikao kilichofanyika kwa dakika 150 kikiwahisisha viongozi wa Yanga, TFF na Serikali.

Katika kikao hicho, Yanga ilipeleka maombi kadhaa kwa Waziri Mwakyembe, ikiwamo uchaguzi wao usimamiwe na kamati ya uchaguzi ya klabu yao, pia ikiomba nafasi nyingine ya kuchukua na kurejesha fomu kwa wagombea wapya, maombi ambayo yalikataliwa na Dk Mwakyembe.

"Mchakato wa uchaguzi wa Yanga huko pale pale, utafanyika Januari 13 kama ulivyopangwa, hatuwezi kutoa nafasi nyingine ya kuchukua fomu kwa wagombea, hao waliochukua pazia limefungwa," alisema Mwakyembe.

Alisema kuhusu ombi la Yanga kutaka kamati yao ya uchaguzi ndiyo isimamie mchakato huo na si TFF ambayo Yanga imeomba ibaki kuwa muangalizi, Dk Mwakyembe amepinga akisisitiza tayari waliwapa nafasi hiyo Yanga na hawakufanya.

"Walipewa siku 75 wafanye uchaguzi hawakufanya, wakapewa siku 60 hawakufanya, isitoshe kamati ya uchaguzi ya Yanga imeshamaliza muda wake, kamati mpya inapaswa kuteuliwa na Kamati tendaji ambayo pia ina wajumbe wanne tu ambao hawawezi kuteua kamati ya uchaguzi.

"Tumekubaliana watusaidie na sisi tuwasaidie, wale watu saba walioteuliwa wa kamati yao ya Uchaguzi, ishirikiane na ile ya TFF ya uchaguzi, mchakato uendelee, kuhusu kurejea kwa Yusuf Manji, hilo haliwezekani, tulishasema kama anahitaji kurejea afuate njia ya uchaguzi tu na huu wa sasa imeshindikana,".

Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema TFF ilikosea kumuondoa Makamu wa rais wa Yanga, Clement Sanga kwenye Bodi ya Ligi kwa kuwa Manji ni Mwenyekiti wa Yanga, kitu ambacho hakikuwa sahihi, ingawa aliikingia kifua TFF akidai imefanya mambo mengi mazuri na hilo kosa moja haliwezi kuharibu mazuri yao.

Akizungumza kwa niaba ya Yanga, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, John Mkwawa alisema kinachohitajika kwa sasa ni utulivu, kipindi hiki wanachoelekea kwenye uchaguzi wa kuziba nafasi zilizokuwa wazi.