Mahadhi akimsikiliza Bushoke atafika mbali

Muktasari:

  • Bushoke amtaka Juma Mahadhi ajaribu kukiokoa kipaji chake kwa kujituma na na aweke umakini pindi anapopewa nafasi ya kucheza

MWANAMUZIKI wa kizazi kipya aliyewahi kutamba na kibao cha Dunia njia, Bushoke amemtaka Juma Mahadhi wa Yanga, ajaribu kukiokoa kipaji chake kwa kujituma na na aweke umakini pindi anapopewa nafasi ya kucheza.

Bushoke amesema amewahi kumfuatilia mchezaji huyo,akiwa kwenye kiwango cha juu na kumuona ana kipaji cha aina yake,hivyo amemtaka kama kuna vitu vinafanya kazi yake ising'ae na kusonga mbele aviweke pembeni kwa muda.

"Kwanza ni mchezaji ninayemkubali kwa kazi zake, ila kwa sasa amekuwa haonyeshi kile kilichotarajiwa na wengi na angekuwa kwenye kiwango kile kile kwa sasa angekuwa nje ya nchi,namshauri kama kuna vitu vinavyofanya kiwango chake kiwe kawaida kawaida tu,aviweke pembeni,"

"Umri alionao ni wakuonyesha ufundi wake na soka limsaidie kujenga maisha yake,akitulia na akaamua anatenga muda kwa ajili ya soka bila shaka litamlipa kwani ana vitu vya ziada,"anasema Bushoke ambaye ni shabiki wa Yanga.