Mtanzania atoa medali ipigwe mnada kujenga ofisi ya RT

Muktasari:

  • Mwanariadha huyo pia atashiriki matembezi ya hisani ambayo yamelenga kukusanya Shilingi 300 milioni zitakazotumika kwa ujenzi wa ofisi za RT.

Arusha. Mshindi namba mbili katika mashindano ya Dunia ya nusu Marathon mwaka 2000, Faustin Baha Sulle ameitoa medali yake aliyoipata ili ipigwe mnada na fedha zitakazopatikana ziende katika ujenzi wa ofisi za Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Mwanariadha huyo alifanikiwa kupata medali ya fedha baada ya kufanya vyema katika mashindano ya Dunia yaliyofanyika katika Jiji la Veracruz nchini Mexico kwa kutumia muda wa saa 1:03:48 huku mshindi wa kwanza alikuwa Paul Tergat raia wa Kenya aliyetumia muda wa saa 1:03:47 na Mthiopia Tesfaye Jifar akimaliza wa tatu kwa muda wa saa 1:03:50.

Anaeleza katika mashindano ya mwaka huo Tanzania iliwakilishwa na wanariadha wawili pekee mwingine akiwa Zebedayo Bayo ambaye alimaliza nafasi ya saba kwa kutumia muda wa saa 1:04:25, ambao walipelekwa na Muitaliano Giano Demadona.

Hata hivyo mwanariadha huyo bado hajatundika daruga na anatarajia kujifua ili kusaka viwango vya kwenda kushiriki mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika mwaka 2020 Tokyo Japan na hapo ndipo atatundika daruga rasmi.

Pia mwanariadha huyo atashiriki katika matembezi hayo “Marathon Walk Across Tanzania” ya siku 30 kutoka Ujiji hadi Bagamoyo yaliyoandaliwa na RT kwa lengo la kukusanya zaidi ya 300 milioni ili kujenga ofisi za RT na kituo cha michezo jambo ambalo limekuwa ni kilio cha wanariadha wengi.