Mwigulu: Singida Utd tukakate miwa tuoteshe alizeti

Muktasari:

  • Singida United imefuzu kucheza fainali ya Kombe La FA kwa kuiondoa JKT Tanzania kwa mabao 2-1, katika mchezo wa nusu fainali.

Arusha. Waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba ameshindwa kuzuia hisia zake baada ya  kuahidi kuisindikiza Singida United hadi Arusha itakapochuana na Mtibwa Sugar katika fainali a Kombe la FA.

Singida United imefuzu kucheza fainali ya Kombe La FA kwa kuiondoa JKT Tanzania kwa mabao 2-1, katika mchezo wa nusu fainali.

Mbunge wa jimbo la Iramba magharibi, Mwigulu amekuwa mdau mkubwa wa soka nchini hasa akizisapoti Singida United, amesema kuwa timu hiyo kufuzu kucheza fainali ni hatua kubwa na anaahidi kuwapa mbinu mbalimbali vijana wake za kuiangamiza Mtibwa.

 “Singida kufikia hatua hii imenipa morali kubwa, sasa kilichobaki na kuwapa mbinu na sapoti kubwa ikiwemo kuwasindikiza Arusha kwa pamoja tukakate miwa tuoteshe alizeti nikimaanisha kurudi na Kombe la FA,” alisema Mwigulu.

Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam inatarajiwa kufanyika jijini Arusha kwenye Uwanja wa Sheik Amri Abeid hapo Juni 2 mwaka huu.

Kombe hilo linaloshikiliwa na Simba SC linatarajiwa kumpata mrithi wake siku hiyo mara baada ya timu hiyo kushindwa kutetea taji lake mbele ya Green Warrious katika hatua za awali huku Yanga nao wakishindwa kutimiza mahitaji yao kwa kombe hilo baada ya kutolewa na Sindida United.

Akizungumzia maandalizi ya mashindano hayo, mwenyekiti soka mkoa wa Arusha, Peter Temu alisema kila kitu kwa sasa kiko sawa wanachosubiri ni mchezo wa fainali.

“Kwa sasa tunamalizia maandalizi machache ya usafi na mazingira ya mapokezi kwa wageni, lakini masuala mengine yote yako sawa,” alisema Temu.