Thursday, September 14, 2017

Ndanda FC waivuruga Mbeya City, yamtimua Kocha Phiri

 

By Justa Musa

Mbeya. Uongozi wa Klabu ya Mbeya City ya jijini hapa umevunja mkataba na aliyekuwa Kocha Mkuu Kinnar Phiri.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Shah Mjanja alisema  kwamba uongozi huo umefikia hatua ya kusitisha mkataba na kocha huyo kutokana na kutoonyesha kuisaidia timu.

Alisema tangu Phiri apokee mikoba kutoka kwa Meja mstaafu  Abdul Mingange, timu imekuwa ikiporomoka kiwango siku hadi siku na kusababisha kupoteza mvuto waliokuwa nao kwa misimu ya  awali.

Mjanja alisema kwa sasa timu hiyo itakuwa chini ya kocha msaidizi Mohamed Kijuso, huku Uongozi ukiendelea na jitihada za kumpata kocha mkuu atakayekiongoza kikosi kwa msimu huu.

Kwa upande wake kocha Phiri alisema anaidai klabu hiyo Sh40 millioni ikiwemo mshahara, posho pamoja na fedha ya mawasiliano waliyokubaliana wakati wa kusaini mkataba huo.

Alisema yeye hatambui kuvunjwa kwa mkataba huo kwani hajalipwa fedha zake ila atalitambua suala hilo baada ya uongozi huo. kumaliza  kumlipa mshahara wa miezi mitatu kuanzia  Septemba hii hadi Novemba mwaka huu.

Alisema" Hadi sasa nipo hapa Mbeya nikisubiri stahiki zangu ambazo natarajia wanilipe ndani ya siku mbili  na endapo nitalipwa zote nami nitakuwa tayari kuvunja mkataba huo na kuyaangalia maisha mengine.

Mbeya City ilifungwa bao 1-0 na Ndanda FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita.

-->