Ndemla, Dilunga waachwa safari ya Simba SC Uturuki

Muktasari:

  • Simba itakuwa Uturuki chini ya kocha Mbeligiji Patrick Aussems akishrikiana na msaidizi wake Masoud Djuma kwa maandalizi Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Dar es Salaam. Simba imewasili salama nchini Uturuki ambapo itaweka kambi mpaka Agosti 5, lakini imewaacha nyota wake Said Ndemla na Hassani Dilunga.

Simba itakuwa Uturuki chini ya kocha Mbeligiji Patrick Aussems akishrikiana na msaidizi wake Masoud Djuma kwa maandalizi Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Nyota wanane wamekosekana katika msafara huo Moses Kitandu, Jamali Mwambeleko, Ally Shomari, Said Mohammed ‘Nduda’, Emmanuel Mseja, ambao huenda wakatolewa kwa mkopo.

Ndemla amebaki kwa kuwa hajatia saini mkataba mpya na huenda akamalizana na klabu hiyo kabla ya Jumatano na kuungana na wenzake Uturuki.

“Hati yangu ya kusafiria ilikuwa na shida lakini imeshakamilishwa na huenda suala langu la mkataba nikamalizana na viongozi siku si nyingi nitasaini mkataba mpya na Jumatano nikaenda Uturuki,” alisema Ndemla.Dilunga ambaye ametia saini mkataba mpya wa kuitumikia Simba hakuwepo katika msafara huo kwa kuwa Simba haijamalizana na Mtibwa Sugar kuhusu fedha ya usajili za kiungo huyo wa zamani wa Yanga.

Mchezaji kiraka Erasto Nyoni hayupo katika msafara huo kwa kuwa ana matatizo ya kifamilia na huenda akajiunga na kikosi hicho wiki hii. Nyoni, mmoja wa mabeki hodari ametua Simba msimu uliopita kutoka Azam FC.