Vijana U-13 yaanza maandalizi mashindano Ubelgiji

Muktasari:

  • Ngorongoro Heroes inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kimataifa dhidi ya Morocco na Msumbiji kabla ya Machi 31 kuwavaa DR Congo katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON-20).

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri  chini ya miaka 13, inatarajiwa kushiriki mashindano ya vijana nchini Ubelgiji yatakayotimua vumbi, Agosti mwaka huu.

Akizungumzia utaratibu sahihi wa kupata kikosi hicho cha vijana, Mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Efram August amesema kutakuwa na mchezo wa kirafiki kati ya Bara na Visiwani.

“TFF inaandaa utaratibu sahihi wa kupata kikosi cha timu ya Taifa kwa vijana wenye umri huo ili kuweza kujiandaa na michuano hiyo ya vijana.

“Tutaanza kwa kucheza mchezo wa kirafiki kati ya Tanzania Bara na Visiwani katika siku za hivi karibuni ili kutoa nafasi kwa walimu kuchagua wachezaji wenye vipaji watakaounda kikosi hicho cha vijana,” alisema mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, Agosti amesema wataanza kutangaza benchi la ufundi kabla ya kuendelea na mchakato huo maalumu utakaotoa nafasi kwa walimu hao kutekeleza majukumu yao.

Wakati huohuo, Ngorongoro Heroes inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kimataifa dhidi ya Morocco na Msumbiji kabla ya Machi 31 kuwavaa DR Congo katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON-20).

Ngorongoro itacheza michezo hiyo ya kuijipima ubavu, Uwanja wa Taifa jijini hapa dhidi ya  Morocco Jumamosi Machi 17 na Machi 21 dhidi ya Msumbiji.