Nigeria yahamisha mechi ya Libya

Muktasari:

  • Nigeria moja ya nchi ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa kisoka kwa sasa barani Afrika, inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na siasa na upinzani wa kisoka unaolikabili Taifa hilo lenye vipaji lukuki vya soka jambo linaloifanya ‘Super Eagles’ kushindwa kutamba katika medani ya soka la kimataifa kutokana na kukosa maandalizi ya mazuri.

Abuja, Nigeria. Shirikisho la soka la Nigeria (NFF), limeamua kuuhamisha mchezo wa kufuzu fainali za Afrika 2019, kutoka uwanja wa Ahmadu Bello mjini Kaduna na kuupeleka mjini Uyo kwa tarehe ileile.

Uamuzi huo umetokana na uwanja huo wa Ahmadu Bello kukosa vigezo baada ya ukaguzi wa kawaida uliofanywa na shirikisho la soka la Afrika (Caf), kuvikagua viwanja mbali mbali barani humo.

Katika taarifa ya NFF, mchezo huo wa kufuzu kwa fainali za Afrika sasa utafanyika kwenye uwanja wa Godswill Akpabio mjini Uyo, baada ya Caf kuukataa uwanja wa Ahmadu Bello, kutokana na pichi yake kuharibika na kuwa hatari kwa wachezaji.

“Nyasi za uwanja wa Ahmadu Bello hazipo kwenye ubora wake na Caf  wameukataa kwa hiyo inatulazimu kuuhamisha mchezo dhidi ya Libya,” ilisema taarifa ya NFF.

Kocha wa Super Eagles, Gernot Rohr, raia wa Ujerumani, alisema uamuzi huo hautaathiri kwa namna yoyote maandalizi ya timu yake kuelekea mchezo huo utakaopigwa mwezi ujao.