Ninje bwana, ameshaanza mambo yake!

Muktasari:

  • Hatua ya mchujo itachezwa hadi Julai kupata timu saba zitakazoungana na Niger kwenye mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Februari 24 hadi Machi 10, mwakan

KOCHA wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, Ammy Ninje amesema kiwango bora cha mabeki, kimechangia kuing’oa DR Congo katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Afrika (Afcon).

Akizungumza kwa simu jana Jumatatu, Ninje amesema ana matumaini ya timu hiyo kucheza fainali za vijana zilizopangwa kuchezwa mwakani nchini Niger.

Ngorongoro iliing’oa DR Congo juzi Jumapili kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya kutoka suluhu ndani ya dakika 90 katika mchezo wa marudiano.

Ngorongoro imetoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Machi 31.

 “Eneo ambalo nilifanyia sana kazi ni ushambuliaji kabla ya mchezo wa marudiano na Congo, lakini  naipongeza safu ya ulinzi kwa kazi nzuri ambayo imeifanya kwenye michezo yote miwili,” anasema Ninje.

Kocha huyo ameongeza kwa kusema ataendelea kuwapa makali washambuliaji kwa kuongeza ‘vitu’ vya kiufundi ili kufanya vyema katika mchezo ujao.

Ngorongoro inatarajiwa kujitupa uwanjani mechi ijao kwa kupepetana na Mali Mei 13 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar

es Salaam kabla ya kurudiana Mei 18.

Hatua ya mchujo itachezwa hadi Julai kupata timu saba zitakazoungana na Niger kwenye mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Februari 24 hadi Machi 10, mwakani.