Nyota Yanga awapa dili madogo

Muktasari:

  • Mkomola alisema nyota wa Serengeti Boys hawapaswi kubweteka na sifa wanazopewa kwa sasa ili kuhakikisha mwakani kama wenyeji wa AFCOn 2019 wanafanya kweli kwa kubakisha taji.

STRAIKA Yohana Mkomola anayekipiga Yanga, ameipa tano Serengeti Boys kwa soka lake katika michuano ya Afcon U17 Kanda ya Cecafa, lakini akaamua kuwauma sikio nyota wake.
Mkomola alisema nyota wa Serengeti Boys hawapaswi kubweteka na sifa wanazopewa kwa sasa ili kuhakikisha mwakani kama wenyeji wa AFCOn 2019 wanafanya kweli kwa kubakisha taji.
Straika huyo aliyekuwa miongoni mwa waoshiriki wa fainali za AFCON 2017 zilizofanyika Gabon, alisema timu hiyo ni kizuri na inacheza soka la kuvutia, jambo linalompa tumaini ya kufika mbali.
“Mimi sina shaka na timu kwani wapo sehemu salama, kikubwa  wafuate maelekezo ya walimu wao lakini pia wajitolee kwa hali na mali, wakifanya hayo timu itakuwa vizuri zaidi kimashindano."
Mkomola aliongeza kwa vile mechi hizi kwao ni maandalizi yao, wachezaji wa Serengeti lazima wajue wana kazi mkubwa mwakani wa kutumia vyema uenyeji wa fainali hizo za Afrika kwa Vijana.