Nyota wa Yanga apata ulaji Misri

Muktasari:

  • Endapo mchezaji huyo atajiunga na klabu hiyo ambayo aligoma kuitaja, atakuwa nyota wa pili kutoka Tanzania kucheza soka nchini humo akitanguliwa na Himid Mao.

Dar es Salaam. Beki tegemeo wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ anatarajiwa kujiunga na klabu ya Ligi Kuu Misri.

Endapo mchezaji huyo atajiunga na klabu hiyo ambayo aligoma kuitaja, atakuwa nyota wa pili kutoka Tanzania kucheza soka nchini humo akitanguliwa na Himid Mao.

Himid aliyekuwa nahodha wa Azam FC, inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, anacheza katika klabu ya Petrojet ya Misri.

Awali, beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, alikuwa akihusishwa kujiunga na Singida United au Azam kabla ya jana kukata mzizi wa fitina.

Akizungumza kwa simu jana, Dante alisema mazungumzo baina yake na klabu hiyo yanaendelea vyema.

“Ndoto yangu ni kucheza soka nje ya nchi na kuja ofa kutoka Misri ni njia ambayo natakiwa kuitumia ili kukamilisha malengo ya kuwa mchezaji wa kimataifa wa Tanzania.

“Sio Misri pekee ambako nina ofa pia Norway, nitaweka wazi klabu gani nitakwenda kujiunga nayo, tuache wasimamizi wangu wafanye kazi yao ya mazungumzo “alisema beki huyo anayecheza nafasi ya mlinzi wa kati.