Oilers yatinga fainali RBA, Savio hakijaeleweka

Muktasari:

Bingwa wa RBA anapata tiketi ya kucheza mashindano ya Majiji Afrika

Dar es Salaam. Klabu ya Oilers imekuwa ya kwanza kutinga fainali ya Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA) huku bingwa mtetezi, Savio ikiwa mguu ndani mguu nje kucheza fainali.

Oilers imetinga hatua hiyo baada ya kuwachakaza maafande wa JKT kwa pointi 70-61 katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali uliofanyika kwenye uwanja wa Bandari, Kurasini matokeo sawa na waliyoyapata kwenye mchezo wa awali.

Ushindi huo mfululizo umeipeleka Oilers moja kwa moja kufuzu kucheza fainali kwani matokeo ya mechi ya tatu baina ya timu hizo hayatakuwa na maana yoyote kwa JKT zaidi ya kuhitimisha ratiba.

Kigingi cha kufuzu kucheza fainali kipo kwa bingwa mtetezi Savio ambaye anahitaji kwa vyovyote vile kushinda mchezo wake wa lala salama leo jioni dhidi ya ABC.

Savio ilifufua matumaini mapya kwenye Ligi hiyo baada ya jana Jumatano kushinda mchezo wa pili wa marudiano kwa pointi 79-72 mbele ya ABC ambayo mchezo wa awali ilishinda 71-57 hivyo timu zote sasa kila moja ina pointi mbili.

Mshindi wa mechi ya leo usiku kati ya Savio na ABC ndiye atafuzu kucheza fainali na Oilers huku timu itakayofungwa ikisaka mshindi wa tatu na JKT.