Ozil aibeba Arsenal ikiichapa Spurs

Sunday November 19 2017

 

London, England. Mesut Ozil amemjibu kocha Arsene Wenger kwa kucheza soka ya uhakika katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham Hotspurs.

Arsenal ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Emirates, ilishinda mabao 2-0 huku Mjerumani huyo akicheza kwa kiwango bora katika eneo la kiungo.

Ozil amekuwa adui wa mashabiki na wachambuzi wa Arsenal wakidai hachezi kwa kiwango bora licha ya kununuliwa kwa bei mbaya kutoka Real Madrid.

Mchezaji huyo alidhibiti la kati akicheza kwa ustadi kwa kutoa pasi murua kwa washambuliaji walioongozwa na Alexis Sanchez.

Sanchez alifunga bao la pili kwa shuti dakika ya 41. Shkodran Mustafi aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa Spurs, alifunga bao la kwanza dakika ya 37.

Sanchez kama Ozil, amekuwa akilalamikiwa na wadau wa soka akidaiwa kutokuwa na msaada katika kikosi hicho.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Chile, amegoma kutia saini mkataba mpya na anahusishwa na mpango wa kujiunga na Manchester City.

Ozil alionyesha ubora wake kipindi cha pili akiwapa raha mashabiki wa Arsenala kwa pasi, chenga mashuti yaliyolenga lango la Spurs.

Hatua ya Ozil kucheza kwa kiwango bora ni majibu kwa Wenger ambaye ameweka bayana kuwa atampiga bei katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Mjerumani huyo amewekwa sokoni, baada ya kugoma kutia saini mkataba mpya na ameanza kuhusishwa na mpango wa kutua Manchester United.

Advertisement