PSG yawawakia Real kwa Neymar

Muktasari:

  • PSG ilimsajili Neymar kutoka Barcelona kwa ada iliyovunja rekodi Dunia, Euro 222 milioni, lakini ndani ya muda mfupi tetesi za kuwa Naymar amepitia huko ili kwenda Santiago Bernabeu zimekuwa zikisikika kila kukicha na kuwaudhi matajiri PSG.

 RAIS wa klabu ya Paris Saint-Germain, Nasser Al-Khelaifi, amekerwa na uvumi na kuamua kuwaendea hewani Real Madrid akiwataka kumthibitishia juu ya ukweli wa taarifa za kutaka kumsajili mshambuliaji wao Neymar.

PSG ilimsajili Neymar kutoka Barcelona kwa ada iliyovunja rekodi Dunia, Euro 222 milioni, lakini ndani ya muda mfupi tetesi za kuwa Naymar amepitia huko ili kwenda Santiago Bernabeu zimekuwa zikisikika kila kukicha na kuwaudhi matajiri PSG.

Al-Khelaifi, alisema kuwa baada ya kuchoshwa na uvumi huo aliamua kuwapigia simu Madrid ili kupata uhakika hasa baada ya televisheni moja ya Hispania kutangaza kuwa wamewasilisha ofa ya Euro 310 milioni ili kumsajili mshambuliaji huyo.

"Hatujafurahishwa na suala hili la Neymar ndiyo maana tuliamua kuwapigia simu viongozi wa Real Madrid, ili kutaka uhakika," alisema Al-Khelaifi.

Hata hivyo Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, alikanusha juu ya suala hilo na akaliweka wazi kwenye mtandao wa klabu hiyo kuwa hawajawahi kuwa na mpango huo licha ya kwamba Neymar ni mchezaji mahiri lakini hawawezi kuwazunguka PSG kiasi hicho.

"Tunajua namna wenzetu walivyoumizwa na suala hili na sijui nini kimetokea na nani waliopika, sisi kama tukimuhitaji mchezaji yeyote kutoka PSG tutawafuata na kuwaambia,” alisema Rais wa Real, Florentino Perez.