Pamba macho yote kwa Arusha United

Muktasari:

  • Timu za Pamba na Arusha United zinatarajiwa kuteremka uwanjani wiki hii kuwania pointi tatu muhimu katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza.
  • Kocha wa Pamba Juma Yusuf, alisema amekiandaa vyema kikosi chake kushinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Mwanza. Kocha wa Pamba Juma Yusuf ‘Simbu’ amesema mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Arusha United utakaochezwa Jumamosi wiki hii utakuwa ni vita.

Yusuf alisema Pamba inatakiwa kushinda mchezo huo ili kuendelea kubaki kileleni katika msimamo wa Kundi B. Timu hiyo ina pointi 11 sawa na Arusha United lakini ina uwiano mzuri wa idadi ya mabao.

“Ni mchezo muhimu kwetu kushinda iwe ugenini au nyumbani, tunaendelea kujiandaa vyema lengo ni kushinda na kubaki katika nafasi nzuri kwenye msimamo,”alisema Yusuf.

Alisema wachezaji wana morali ya kufanya vyema katika mchezo huo, baada ya kutoka sare na Geita Gold katika mchezo uliopita.

Pamba iliwahi kutamba katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara (zamani Daraja la Kwanza) enzi hizo ikiundwa na wachezaji nyota waliotamba katika soka.