Pasi zamtoa Boban Lyon

Dar es Salaam. Kiwango alichokionyesha kiungo wa zamani wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ kwenye mchezo dhidi ya Lipuli, iliyopigwa Novemba 2 mwaka huu, ndiyo iliyompa ulaji wa kujiunga na Yanga.

Boban alijiunga na Yanga juzi kwa mkataba wa miezi sita, siku chache baada ya kumwagiwa sifa na kocha wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera, kuwa ni mchezaji mwenye hesabu nzuri pindi awapo uwanjani.

Boban alionyesha uwezo mkubwa kwenye mchezo huo, ambao aliisaidia kwa mara ya mwisho, African Lyon kuibuka na ushindi kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam akipiga pasi mbili matata.

Kiungo huyo alifunga bao la kwanza kwa African Lyon kwa mpira wa adhabu ulioenda moja kwa moja nyavuni mwa Lipuli wakishinda kwa mabao 2-0.

Akizungumza sababu za kumsajili Boban, Zahera, alisema kwa mara ya kwanza alimuona Boban kupitia luninga na ilikuwa Jumatatu ya Oktoba Mosi wakati timu yake ikicheza na JKT Tanzania.

Katika mchezo huo, African Lyon, ilipoteza kwa bao 1-0 ugenini kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Samuyo, uliopo Mbweni, jijini Dar es Salaam, na Boban alionyesha kiwango cha juu.

“Nilimuona Boban kwenye televisioni akipiga pasi kama mbili hivi kwenye mchezo huo, ambazo zilinifanya nitambue kuwa ni mchezaji wa tofauti, ana uwezo wa kufanya makubwa.

“Nilivutiwa pia na namna alivyokuwa na uamuzi wa haraka akiwa na mpira, ndio maana nikawaambia viongozi wa Yanga wamsajili,” alisema.

Kiungo wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe ambaye aliwahi kucheza na Boban, alisema Yanga wamelamba dume, kwani Boban ni bonge moja la mchezaji tena wa kiwango cha juu nchini.