Pogba atupia mbili, Ronaldo alimwa kadi nyekundu

Muktasari:

  • Tangu msimu uliopita hakuna beki aliyehusika kutegeneza mabao mengi ya Ligi ya Mabingwa zaidi ya beki wa kushoto wa Real Madrid, Marcelo (amefunga mabao matatu, na kutegeneza matano).

London, England. Kiungo wa Manchester United, Paul Pogba ameonyesha ubora wake kwa kuiteka Uswisi, wakati Cristiano Ronaldo akitolewa nje kwa kadi nyekundu Hispania na Manchester City ikichezea kichapo nyumbani katika michezo ya jana ya Ligi ya Mabingwa.

Mabingwa watetezi Real Madrid imetoa kipigo kizito cha mabao 3-0 kwa Roma na kuonyesha kuwa wapo tayari kwa maisha yao bila ya Ronaldo.

Young Boys 0-3 Manchester United

Paul Pogba alifunga mabao mawili, huku bao lake la kwanza akifunga kwa juhudi binfasi, wakati vijana Jose Mourinho wakipata ushindi mwepesi nchini Uswisi. Kipindi cha pili Pogba alitegeneza bao la tatu lililofungwa na Anthony Martial na kuwaweka kileleni Man United.

Shakhtar Donetsk 2-2 Hoffenheim

Hoffenheim mara mbili wameongoza kupitia mabao ya  Havard Nordtveit, lakini wamefanikiwa kuvuna pointi moja tu ugenini Ukraine baada ya wenyeji kusawazisha katika dakika 81, kupitia chipukizi wa Brazil, Maycon de Andrade Barberan.

Benfica 0-2 Bayern Munich

Robert Lewandowski alifunga bao la kuongoza dakika 10, kabla ya kiungo Renato Sanches kupachika bao la pili kwa Bayern wakipata ushindi mzuri kwenye Uwanja wa Da Luz.

Real Madrid 3-0 AS Roma

Real Madrid imeanza kutetea vizuri taji lake kwa kupata ushindi mzuri nyumbani dhidi ya Roma.

Real ilipata bao la kwanza lililofungwa na Isco kwa shuti la umbali wa mita 25, huku Gareth Bale akiongeza la pili kabla ya Mariano Diaz kupachika la tatu kwa shuti la umbali wa mita 20.

Manchester City 1-2 Lyon

Manchester City imeanza vibaya Ligi ya Mabingwa baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Lyon kwenye Uwanja wa Etihad.

Maxwel Cornet alifunga bao la kwanza kwa Wafaransa hao akiunganisha krosi ya Nabil Fekir. Nahodha Fekir alifunga bao la pili kabla ya Bernardo Silva kufunga bao la kufutia machozi kwa City akimalizia vizuri kazi ya Leroy Sane.