Pogba na wenzake wajitoa Ufaransa ikiivaa Uholanzi

Muktasari:

  • Wachezaji wanne wamejitoa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ufaransa kinachojiandaa kwa mechi ya Nations Ligi dhidi ya Uholanzi na mchezo wa kirafiki dhidi ya Uruguay.

Paris, Ufaransa. Wachezaji wanne akiwemo Paul Pogba wamejiondoa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ufaransa inayojiandaa na mchezo dhidi ya Uholanzi.

Kocha Didier Deschamps aliwaita wachezaji hao kwa ajili ya mechi mbili dhidi ya Uholanzi wa Nations Ligi na ule wa kirafiki dhidi ya Uruguay zitakazochezwa IJumaa na Jumanne ijayo.

Wachezaji walijiengua kutoka kwenye kikosi hicho kwa sababu mbali mbali zinazotokana na majeruhi wengine wakiwa mshambuliaji Anthony Martial wanaocheza Manchester United, beki Benjamin Mendy wa Manchester City na mshambuliaji wa Arsenal Alexandre Lacazette.

Martial amekuwa kwenye kiwango bora kwa sasa ndiye aliifungia Man United bao la kufutia machozi kwa penalti ilipocheza na Man City na kufungwa 3-1 Jumapili iliyopita.

Pogba yeye hakucheza mchezo huo wa kichapo kutoka kwa Man City kama ilivyo kwa Martial anasumbuliwa na nyama za paja wakati Mendy akiugulia maumivu ya goti.

Lacazette yeye anasumbuliwa na nyonga na nafasi ya Pogba imechukuliwa na kiungo wa Tottenham, Moussa Sissoko huku ile ya Matial ikichukuliwa na mshambuliaji wa Borussia Monchengladbach fya Ujerumani, Alassane Plea, 25.

Aidha nafasi ya Benjamin Mendy, imechukuliwa na mdogo anacheza kwenye klabu ya Lyon, Ferland Mendy mwenye miaka 23, ambaye ameitwa kwa mara ya kwanza.

Chama cha soka Ufaransa kimesema kuwa kiliwasiliana na madaktari wa Arsenal na kufahamishwa kuwa Lacazette asitumiwe kwa kuwa anapata matibabu.

Ufaransa itaifuata Uholanzi mjini Rotterdam, Ijumaa ya Novemba 16 kabla ya kucheza na Uruguay kwenye Uwanja wa Stade de France, Jumanne ijayo Novemba 20.