Pointi za Yanga ziko shakani

Muktasari:

  • Hata hivyo kosa la kwanza halikuwa kuzidisha idadi ya wachezaji, isipokuwa ni kuendelea kucheza kwa mchezaji aliyefanyiwa mabadiliko.

WAKATI  macho na masikio ya mashabiki wa Yanga yameelekezwa Kamati ya Bodi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72), uwezekano wa klabu hiyo kuvuna pointi za mezani upo shakani.

Yanga imekata rufani kupinga matokeo ya mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Hussein Nyika amedai kuwa wamewasilisha malalamiko dhidi ya Mbeya City kwa kumuingiza mchezaji ambaye alikuwa amefanyiwa mabadiliko na akaendelea kucheza.

Pia Nyika amedai mchezaji wa Mbeya City aliyepewa kadi nyekundu alirejea uwanjani na kushangilia na wenzake, jambo ambalo ni makosa kwa mujibu kanuni.

Hata hivyo, Yanga haina matumaini ya moja kwa moja itapata ushindi kupitia rufani yake kutokana na mazingira ya kanuni za soka nchini.

Kanuni ya Ligi Kuu Bara inayoweza kuwabeba Yanga kulingana na mazingira ya tukio hilo ni ya 14 (25) inayoeleza namna timu inavyoweza kupewa ushindi wa mezani kutokana na makosa ya kumbadilisha mchezaji.

"Timu inaruhusiwa kubadilisha wachezaji watatu (3) tu katika mchezo mmoja,wanaoingia mbadala ni lazima watokane na orodha ya wachezaji 7 (saba) wa akiba,

Timu itakayozidisha kwa kubadilisha zaidi ya wachezaji watatu (3) itapoteza mchezo husika na kutozwa faini," inafafanua kanuni hiyo.

Hata hivyo kosa la kwanza halikuwa kuzidisha idadi ya wachezaji, isipokuwa ni kuendelea kucheza kwa mchezaji aliyefanyiwa mabadiliko.

Kosa la pili ambalo Yanga imekata rufani ni kurejea uwanjani kwa mchezaji aliyeonyeshwa kadi nyekundu ambalo ni uvunjaji wa kanuni ya 14(44) ambayo hata hivyo adhabu yake sio timu pinzani kupewa pointi kwa mujibu wa kanuni ya 14(49).

"TFF/TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wowote wa taratibu za mchezo kama zilivyoainishwa kwenye kanuni ya 14 kwa kutoa onyo kali au karipio au kutoza faini kuanzia Sh200,000 mpaka Sh3 milioni au kufungiwa  michezo isiyozidi mitatu (3) au kipindi kisichozidi miezi mitatu (3) kwa mchezaji, kiongozi au timu," inafafanua kanuni hiyo.

Akizungumzia mkanganyiko huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Chama alisema kwa mujibu wa kanuni makosa hayo hayasababishi matokeo ya mchezo kubadilika.

"Suala la mabadiliko ya mchezaji anayesimamia ni mwamuzi wa akiba ambaye kama kuna tatizo lolote anapaswa kumjulisha mwamuzi wa kati ili hatua zichukuliwe, hivyo kama kuna tatizo likibainika nadhani mwamuzi wa akiba ndiyo atawajibishwa.

“Lakini kuna Kamati ya saa 72 inayofuatilia na kutoa uamuzi wa masuala yote yanayohusu ligi, kamati itakaa na kupitia ripoti ya refa na vielelezo vingine na kama kuna hatua zozote za kumchukulia mwamuzi itatujulisha lakini kimsingi hilo halifanyi matokeo ya mchezo yabadilike," anasema Chama.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Waamuzi  Tanzania (FRAT), Oden Mbaga amesema kuwa endapo mwamuzi wa mchezo amegundua kuna mchezaji amezidi uwanjani, anapaswa kusimamisha mchezo na kuamuru atolewe.

Pia mwamuzi anapaswa kuipa timu pinzani pigo kubwa kwa kuangalia eneo ambalo mpira ulikuwepo wakati mchezaji aliyezidi alipoingia.

“Kama aliingia wakati timu yake inashambuliwa na mpira ulikuwa kwenye eneo la hatari, timu pinzani itapewa penalti na mchezaji husika ataonyeshwa kadi ya njano, lakini ukiwa sehemu tofauti na eneo la hatari, mchezaji husika atapewa kadi ya njano,"anasema Mbaga.

“Wapinzani watatakiwa kupiga faulo, lakini bado haiwezi kuathiri matokeo ya mchezo ikibainika refa alikosea japo yeye mwamuzi na yule wa mezani watapaswa kuadhibiwa ikibainika ni makosa yao."

 

KAULI ZA YANGA

Katibu wa Yanga, Charles Mkwasa amedai Mbeya City inatakiwa kuwajibishwa kwa mujibu wa kanuni baada ya kuanzisha vurugu sanjari na kumuingiza mchezaji katika mazingira ya kutatanisha.

 “Mbeya City wanatakiwa kuwajibishwa kwa vurugu walizofanya mashabiki wao kurusha mawe, siyo uungwana,” anasema Mkwasa.

 

Msikie Leslie Liunda sasa

Mwamuzi nguli wa zamani, Leslie Liunda alisema hawezi kutoa kauli kuhusu sakata hilo kwa kuwa ni mjumbe wa Kamati ya Saa 72.

“Naomba kutafutwa baada ya kikao cha Kamati ya Saa 72, wasiwasi wangu naweza kutoa maelezo yanayoweza kuleta utata ni bora tusubiri,” anasema Liunda.