Polisi wamwagwa makao makuu ya TFF kuimarisha ulinzi katika maandalizi uchaguzi wa shirikisho hilo

Muktasari:

Maofisa hao ambao ni Polisi waliovaa sare, askari kanzu, maofisa wa idara ya usalama wa taifa pamoja na wale wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wamekuwa hawabanduki ndani ya ofisi hizo.

 Katika kile kinachoonekana Serikali kuufuatilia kwa ukaribu mchakato wa uchaguzi wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama vimepiga kambi katika makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo Karume jijini tangu Ijumaa.

Maofisa hao ambao ni Polisi waliovaa sare, askari kanzu, maofisa wa idara ya usalama wa taifa pamoja na wale wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wamekuwa hawabanduki ndani ya ofisi hizo.

Mwanzoni Ijumaa na Jumamosi, askari Polisi waliovaa kiraia tu ndio walikuwa wanadumisha ulinzi kwenye eneo hilo, lakini leo Jumatatu, tumeshuhudia polisi wenye sare na maofisa wa usalama wa taifa na Takukuru wakipiga kambi kufuatilia kwa ukaribu zoezi la uchukuaji fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.

Hali hiyo imeonekana kuzuia hofu kubwa kwa wafanyakazi wa TFF ambao wamekuwa makini katika kufuatilia na kuzungumza na wageni mbalimbali wanaofika kwenye ofisi hizo.

"Hapa askari Polisi wenye sare na waliovaa kiraia wamesambaa kila kona ukijumlisha na watu wa usalama wa taifa na Takukuru ambao wanafuatilia kila kinachoendelea.

Huu uchaguzi wa safari hii serikali iko makini nao kupita kiasi na ndio maana kila mmoja wetu hapa anafanya kazi akiwa na presha kubwa," alisema mmoja wa wafanyakazi wa TFF ambaye hakupenda kutajwa jina.

Uchukuaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa shirikisho hilo linatarajiwa kufungwa rasmi leo huku uchaguzi huo ukitarajiwa kufanyika mkoani Dodoma, Agosti 12.