Rais wa Fifa apinga Barca, Girona kupigwa Marekani

Muktasari:

  • Infantino Fifa alisema amezisikia taarifa hizo za mchezo huo baina ya Girona na Barcelona kutaka kuchezwa Uwanja wa Hard Rock mjini Miami, Januari 26 mwakani.

Zurich, Uswisi. Rais wa Shirikisho la soka la kimataifa (Fifa), Gianni Infantino, amejitokeza kupinga mpango wa kuchezea mechi za Ligi Kuu Hispania nchini Ufaransa ukiwemo mchezo wa kwanza baina ya Girona na Barcelona.

Infantino Fifa alisema amezisikia taarifa hizo za mchezo huo baina ya Girona na Barcelona kutaka kuchezwa Uwanja wa Hard Rock mjini Miami, Januari 26 mwakani.

“Kwangu mimi ningefurahi kuona mchezo baina ya Girona na Barcelona unachezwa Estadi Montilivi badala ya Marekani na mechi za Ligi Kuu Marekani zikapigwa nchini humo na sio vinginevyo,” alisema.

Bosi huyo wa soka alionekana kuwashangaa bodi inayoendesha Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, kufikiria kuhamishia Ligi ya nchi hiyo Marekani badala ya kuangalia namna ya kuiboresha.

Infantino alisema ili uamuzi huo wa La Liga uweze kufanya kazi ni lazima Shirikisho la soka Hispania na Marekani ziidhinishe sawa na Shirikisho la soka Ulaya (Uefa) pamoja na lile la Amerika ya Kaskazini na Kati (Concacaf), pamoja na Fifa.

“Hili haliwezi kwenda kirahisi kama wanavyodhani lazima mamlaka husika ziidhinishe pamoja na kupata Baraka za Fifa,” alimalizia Infantino.

Akionekana kuchomwa na kauli ya Infantino, Rais wa La Liga, Javier Tebas, aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba anamshangaa bosi huyo wa Fifa kujaribu kuwawekea kauzibe wakati hajazuia timu za Canada kushiriki Ligi ya Marekani.

“Kwa sasa Toronto ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Marekani timu hiyo pamoja na Montreal na Vancouver zinashiriki Ligi hiyo wakati Canada pia kuna Ligi nyingine inachezwa kwa nini asizuie kwanza hizo," alihoji.

La Liga imevuna mamilioni ya dola kutokana na uamuzi huo wa kuhamishia mechi moja ya nyumbani ya kila timu ya Hispania kuchezwa Marekani, baada ya kuingia mkataba wa miaka 15 na Kampuni ya televisheni ya Relevent.

Aliyekuwa Kocha wa timu ya Taifa ya Hispania ambaye kwa sasa anainoa Real Madrid, Julen Lopetegui, alikuwa wa kwanza kupinga mpango huo wa La Liga akiuona  hauna tija katika mustakabali wa soka la Hispania.