Rais wa Fifa atua nchini

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe leo Alhamisi akiongozana na Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Rashid Ali Juma amempokea Rais wa Shirikisho la Mpira Duniani (Fifa), Gianni Infatino ambaye aliongozana na Rais wa CAF, Ahmad Ahmad, Rais Fifa na ujumbe aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 10:20 alfajiri. Waziri Mwakyembe amemhakikishia Rais wa Fifa utayari wa Tanzania katika kushirikiana na kutekeleza miradi na mipango mbalimbali ya Fifa. Aidha, Waziri Mwakyembe alimhakikishia Rais wa Fifa kwamba Mkutano huo wa Fifa utafanyika kwa amani na kwamba Watanzania wanawakaribisha kuja kujionea vivutio vilivyopo nchini. Waziri Mwakyembe alimtaarifu Rais wa Fifa kuhusu mapokezi rasmi yatakayofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye yupo safarini. Kwa upande wale, Rais wa Fifa alimshukuru Waziri Mwakyembe kwa mapokezi mazuri aliyopata.

 Rais wa Fifa alimhakikishia Waziri Mwakyembe ushirikiano katika masuala mbalimbali ya mpira wa miguu.  Aidha, Rais wa Fifa alisema chaguo la kufanyia mkutano huo Tanzania limetokana na maendeleo ya kasi ya tasnia ya mpira wa miguu na weledi wa viongozi wa TFF waliopo madarakani.