Straika wa Lyon aibuka mfungaji bora Coastal Union

Muktasari:

  • Aifungia Coastal Union mabao nane katika michezo kumi na nne aliyocheza.

STRAIKA Raizin Hafidh aliyekipiga msimu uliopita katika klabu ya Afrikan Lyon, ameibuka mfungaji bora wa Coastal Union baada ya kuifungia timu hiyo mabao nane katika michezo kumi na nne aliyocheza.

Mchezaji huyo alisema alikuwa na lengo la kuhakikisha anatengeneza historia nzuri akiwa na kikosi hicho ili kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza.

"Ujue mimi nilikuwa hapa katika kikosi cha vijana kabla ya kuondoka na kwenda Lyon, hivyo nilivyorudi tena hapa, nilipanga kufanya kitu kikubwa ambacho kitanifanya nijihakikishie namba na nimefanikiwa," alisema.

Raizin alisema aliamua kuondoka Coastal baada ya kukosa nafasi ya kucheza baada nafasi yake kuwa na Haroun Moshi 'Boban', ambaye alikuwa katika kiwango kizuri.

"Nafasi yangu alikuwa nacheza Boban, ilikuwa ngumu mimi kupandishwa na kucheza nafasi ile, nikabidi niende sehemu ambayo nitacheza ndio nikatua Lyon, lakini leo nimerudi na nimekuwa mfungaji bora wa timu ni jambo zuri kwangu," alisema.

Aliongeza kwamba moto wake huo anataka kuuhamishia katika ligi kuu ili kuzidi kujitengenezea jina.