Rashford asema England hakuna kulala

Muktasari:

  • Rashford aliweka picha kwenye mtandao wake ikimuonyesha akifanya mazoezi binafsi kujiandaa na fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni 14.

London, England. Mshambuliaji kinda wa England, Marcus Rashford, amepania fainali za Kombe la Dunia nchini Russia.

Rashford aliweka picha kwenye mtandao wake ikimuonyesha akifanya mazoezi binafsi kujiandaa na fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni 14.

Licha ya kikosi cha England kupata mapumziko mafupi, mchezaji huyo mwenye miaka 20, alifanya mazoezi kujiweka fiti kwa mashindano hayo.

“Siku chache za mapumziko natakiwa kuongeza kasi kujiweka fiti kwa majira ya kiangazi,” aliandika Rashford.

Kinda huyo amepania kurejesha makali baada ya kushindwa kung’ara msimu huu kwenye kikosi cha Manchester United.

Jose Mourinho amekuwa akishutumiwa na baadhi ya nyota wa zamani wa timu hiyo akiwemo Paul Scholes kwa kumuweka benchi.

“Wachezaji chipukizi kama hawa wanahitaji kuungwa mkono, mapenzi lakini hawapati. Hawawezi kukuza kiwango chao katika mazingira kama haya,” alisema Scholes.

Nguli huyo ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, anatajwa mmoja wa viungo bora waliowahi kutokea Man United na England.