Rekodi kocha mpya Simba usipime, yampa raha Taifa

Muktasari:

  • Lechantre, aliishuhudia Simba ikipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 Timu ya Simba imempa mapokezi ya aina yake kocha mpya Pierre Lechantre, baada ya jana kumpa zawadi ya mabao katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lechantre, aliishuhudia Simba ikipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, alifunga mabao mawili katika mchezo huo. Okwi anaongoza kwa ufungaji baada ya kufikisha mabao 10.

Mfaransa huyo alikuwa jukwaani akiangalia vijana wake walioongozwa na msaidizi wake Mrundi Masoud Djuma, wakicheza soka ya kutakata dakika zote 90 za mchezo huo.

Lechantre anatarajiwa kujaza nafasi ya Mcameroon Joseph Omog ambaye Simba ilimtupia virago na Djuma kupewa jukumu la kuingoza timu hiyo kwa muda akisubiriwa kocha mkuu.

Simba jana ilicheza soka maridadi katika idara zote huku libero mpya Mghana Asante Kwasi, akicheza kwa ustadi mchezo huo sanjari na kufunga bao la pili na jingine likiwekwa wavuni na Shiza Kichuya.

Hata hivyo, Lechantre anakabiliwa na kazi ngumu ya kuvunja mfupa uliowashinda makocha wanane ndani ya kipindi cha miaka mitano cha kushindwa kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara tangu msimu 2011-2012.

Tangu Simba ilipotwaa ubingwa 2011/2012 chini ya kocha Milovan Cirkovic, timu hiyo imejikuta ikigeuka mnyonge mbele ya Yanga iliyotwaa mara nne ikipokezana na Azam FC iliyonyakuwa mara moja.

Makocha waliomtwisha zigo Lechantre wa kuipatia Simba ubingwa wa Ligi Kuu ni Patrick Liewig, Abdallah Kibadeni, Zdravko Logalusic, Patrick Phiri, Goran Kopunovic, Dylan Kerr, Jackson Mayanja na Joseph Omog.

Sikia rekodi ya Lechantre

Mafanikio ya Lechantre katika soka la Afrika yameivutia Simba. Kocha huyo ana rekodi nzuri katika maeneo tofauti duniani kwa muda wa miaka 31, lakini pia amecheza soka kwa miaka 19 katika timu za Sochaux, Monaco, Laval, Lens, Marseille, Reims, Red Star na Paris FC. Kocha huyo amefundisha soka Afrika kwa miaka 16 kwenye ngazi ya klabu na timu ya Taifa na ametwaa mataji kadhaa.

Katika ngazi ya klabu Afrika, Lechantre amezinoa timu za Al-Ettihad Club Tripoli ya Libya, CS Sfaxien na Club Africain (Tunisia) na MAS Fes ya Morocco.

Timu za Taifa, amezinoa Mali, Congo na Cameroon ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika (Afcon) yaliyofanyika Nigeria mwaka 2000.

Kocha huyo pia aliiongoza Club Africain kumaliza nafasi ya pili ya Ligi Kuu Tunisia mwaka 2009 na 2010 huku pia akiiwezesha klabu hiyo kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika ya Kaskazini mwaka 2010.

Klabu nyingine ni Al Ahli ya Saudi Arabia na Al Arabi, Al Rayyan, Al-Siliya Sports Club (Qatar) lakini pia amewahi kufundisha timu ya Taifa ya Qatar.

Pambano lenyewe Taifa

Simba ilianza vyema mchezo na dakika ya tatu ili.pata bao la mapema lililofungwa na Kichuya akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Mwinyi Kazimoto.

Dakika 22 Simba inafanya mabadiliko kwa kumtoa Kazimoto na kuingia Said Ndemla na dakika moja baadaye alipenyeza pasi kwa Kwasi aliyefunga bao la pili.

Simba ilitumia mfumo wake wa 3-5-2 uliojaza viungo wengi Jonas Mkude, James Kotei, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Nicholas Gyan ambaye alikuwa anacheza kama winga wa kulia.

Okwi aliyeingia kuchukua nafasi ya Mzamiru alifunga bao la tatu dakika ya 76 kabla ya kupiga la nne dakika ya 82.