Riadha miaka 20 medali saba tu

Muktasari:

Takwimu za Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) zinaonyesha kuwa tangu mwaka 1997 hadi Machi mwaka huu, wanariadha 130 waliwakilisha nchi katika mbio mbalimbali, huku wakirudi na medali za kimataifa saba pekee.

Dar es Salaam. Kwa takriban miaka 20 sasa, Tanzania imekuwa ikisuasua katika riadha, licha ya Shirikisho la Riadha nchini (RT) kupeleka timu kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Michezo ya Olimpiki, Afrika, Madola na ubingwa wa dunia na mbio za nyika.
Takwimu za Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF) zinaonyesha kuwa tangu mwaka 1997 hadi Machi mwaka huu, wanariadha 130 waliwakilisha nchi katika mbio mbalimbali, huku wakirudi na medali za kimataifa saba pekee.
Kati ya medali hizo saba, nne za dhahabu zilibebwa na Restituta Joseph, Samson Ramadhan, Fabiano Joseph na Alphonce Simbu.
Dhahabu hizo zilianza kupatikana mwaka 2001 baada Restituta, ‘binti’ wa Singida, kushinda katika Mbio za Nyika za dunia. Joseph aliitwaa dhahabu katika mbio za dunia mwaka 2007, Ramadhan (Jumuiya ya Madola, 2006 na Simbu aliyeshinda mashindano ya Standard Chartered Mumbai Marathon Januari mwaka huu.
Mbali na dhahabu, wanariadha wa Tanzania waliwahi kushinda medali mbili za fedha na shaba moja kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na medali walizovuna Kenya ndani ya kipindi hicho.
Pamoja na wingi huo wa wanariadha, uchambuzi wa Mwananchi umebaini kuwa robo tatu ya wanamichezo hao wamekuwa wakitoka kwenye mikoa miwili tu ya Singida na Manyara jambo linaloonyesha kuwa mikoa mingine hakuna uwekezaji wa kutosha katika mchezo huo.
Kati ya wanariadha hao, 52 ni wazaliwa wa Singida na 40 wa Manyara huku 38 waliosalia wakitokea mikoa ya Arusha, Dodoma, Mara na Mbeya huku Dar es Salaam yenye wakazi takriban milioni tano, ikikosa kabisa uwakilishi katika kipindi hicho.
Manyara na Singida hazijawa kitovu cha riadha nchini kwa bahati mbaya. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu katika mikoa hiyo, umebaini kuwa mchezo huo ni sehemu ya maisha ya wakazi wa mikoa hiyo huku baadhi ya familia zikiwa tayari kuwapeleka watoto wao katika vituo maalumu kukuza vipaji vyao.
Tofauti na mikoa mingine kama Dar es Salaam, ndani ya Manyara na Singida hasa vijijini ni nadra kuwaona watoto wakicheza mpira wa miguu badala yake sehemu kubwa hushiriki michezo ya kukimbia na kulenga shabaha.
Siri ya ushindi

Mfumo wa maisha ya wakazi wa mikoa hiyo, mazingira, mila, desturi na imani vinatajwa na wenyeji kuwa kuchochea mikoa hiyo kuibeba riadha ya Tanzania kwa miaka mingi.
“Vijana wetu hutembea umbali mrefu kutafutia mifugo malisho na watu wazima hutembea kilomita nyingi wanapokwenda mashambani,” anasema Turuway Aweso, mkazi wa Kijiji cha Gedamali, Babati mkoani Manyara.
“Hata wanafunzi nao wanapoenda shuleni hutembea umbali mrefu kuliko kawaida hivyo mazingira yanatulazimisha kufanya mazoezi bila kujua.”
Huku akionyesha eneo la kijiji hicho ambacho kina mazingira rafiki kwa wakimbiaji, Aweso anasema mambo hayo yakijumlishwa na shughuli za uwindaji, yanachangia moja kwa moja mkoa huo kutoa wanariadha nyota nchini.
“Sehemu kubwa ya Gedamali, ambako wanatokea Joseph na mwanariadha wa zamani, Gidamisi Shahanga, ni tambalale na wakati natembelea kijiji hicho mwanzoni mwa Machi kulikuwa na baridi kali na upepo wa kupausha.”
Maisha yalivyo Gedamali
Kutokana na umbali hadi kufika shuleni, wanafunzi wengi wa kijiji hicho asubuhi kutembea kilomita nane hadi 10 kwa safari moja hivyo sehemu kubwa hulazimika kukimbia ili kuwahi vipindi darasani na jioni kupeleka mifugo malishoni. “Mazingira kama hayo ndiyo yalinishawishi niingie kwenye riadha, nilikuwa nikikimbizana na wanyama nilipokuwa nikiwapeleka malishoni,” anasimulia Joseph ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za nusu marathoni.
Riadha ni mchezo mkuu hata katika shule za msingi za Singida na Manyara na walimu wamewajengea mtazamo wanafunzi wao kwamba ili kuanza siku vizuri na kujifunza kwa ufanisi, lazima wakimbie mchaka mchaka kabla ya kuanza vipindi.
“Tunafundishwa riadha shuleni, mwalimu wetu wa michezo hutueleza kwamba mchezo huu unaweza kutufanya kuwa matajiri kwa muda mfupi sana, binafsi napenda sana kukimbia,” anasema Neema Saktay (16) anayesoma darasa sita katika Shule ya Msingi Gedamali.

Hata wakati walimu wakiwajengea watoto kuwa riadha inawaongezea uwezo wa kujifunza, wazazi huwashawishi watoto kuupenda mchezo huo ili siku zijazo uwakomboe kiuchumi.

“Ni rahisi kupata mafanikio ya riadha kwa muda mfupi hasa kipindi hiki ambacho mkimbiaji kuvuna mpaka milioni 100 katika mbio moja ndani ya dakika 30 inawezekana,” anasema John Steven Akhwari wa Manyara.

Mbali na shughuli za kawaida, baadhi ya wananchi wamejitolea kujenga vituo vya kukuzia vipaji kama alivyofanya Jambao Madai, mkazi wa Mampando, Ikungi mkoani Singida.

“Vijana walikuwa wakishiriki riadha bila malengo, wengi walikimbia kama njia ya kutekeleza kwa haraka majukumu yao nikapata wazo kwanini tusiwasaidie kwa kuanzisha kituo maalum cha kuwapa mafunzo.

“Tulianza kidogo kidogo kwa kuwakusanya vijana wenye vipaji na kuwafundisha lakini hawakuwa kambini,” anasema Jambao ambaye amejenga kituo cha vyumba viwili.

Licha ya hali ya kituo hicho kuwa katika mazingira magumu, kimesaidia kuwatoa mastaa lukuki wa riadha wanaotokea mkoa huo akiwemo Simbu.

Jambao hutumia fedha zake zinazotokana na mazao kuwagharamia watoto wapatao 20 wanaoishi katika kituo hicho huku wengine wakiendelea na masomo yao.

Pale anapokwama, wazazi wa watoto huchanga vyakula na fedha zinazoweza kumsaidia kuendelea kuwapa mafunzo watoto hao ili waje kuwa wanariadha mashuhuri. Simbu ni miongoni mwa mastaa waliopitia kituo hicho.

Mbali na hamasa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la riadha Tanzania (RT), Dk Hamad Ndee anasema mazingira ya mikoa hiyo ambayo bonde la ufa limepita yameisaidia mikoa hiyo kuwa chimbuko la riadha nchini.

Lakini pia katibu wa Chama cha riadha Singida, Benno Msanga anataja asili ya watu wa mikoa hiyo kuwa na chembechembe za riadha.

“Jografia na baiolojia ya wazaliwa wa Singida ndiyo chanzo cha kutoa wanariadha wengi nchini, asili ya Wanyaturu ni Ethiopia, hawa ni Wahabeshi, hata tabia yao na waethiopia zinaendana kwani ukanda huu limepita bonde la ufa hadi Ethiopia,” anasema Msanga.

John Paret (70) mkazi wa Katesh ambaye ni mmoja wa wazee wa kimila, anasema mbali na jiografia ya mikoa hiyo kuwa chanzo cha wakazi wake wengi kuwa wakimbiaji, vilevile aina ya vyakula, imani na nidhamu ya mchezo pia vimechangia.

“Vyakula tunavyokula ni vya asili, mfano hapa Singida, tunakula mtama, uwere, mlenda na maziwa, hicho ndicho chakula chetu kikuu, chakula hiki kinachangia kutujengea nguvu, lakini pia wenzetu wa Manyara wanakula vyakula vya asili vya mizizi,” anasema.

Ukiachana na vyakula, nidhamu imechochea vijana wengi kufanikiwa katika riadha.

“Nidhamu ya mazoezi, hakuna asiyejua misimamo ya watu wa huku, lakini katika suala la mazoezi wako makini sana, hawaoni shida kukimbia, hiyo ndiyo furaha yao kwa kuwa wamejijengea tabia hiyo tangu wadogo,” anasema.

Hata wakati mikoa mingine ikiwa nyuma katika mchezo na hata kushindwa kutoa wawakilishi ndani ya timu ya Taifa, Singida na Manyara inaenda kujiimarisha ili kuhakikisha wanariadha wake siyo tu wanashiriki michuano ya kimataifa bali wanarudi na medali nyingi za dhahabu.

Mwenyekiti wa riadha Manyara, Safari Ingi anasema tayari wamekutana na Serikali ya mkoa na sasa wako katika harakati za kuchagua ni wilaya ipi kijengwe kituo cha riadha cha mkoa ambacho kitatoa fursa kwa wanariadha wa mkoa huo kujifua na kuendeleza vipaji vyao.

Wakati Manyara wakijipanga, Mwenyekiti wa riadha Singida, Benno Msanga anasema mpango wa kujenga kituo bado haujafanikiwa kutokana na kutokuwa na rasilimali fedha lakini kama Chama kimekuwa kikiunga mkono juhudi za baadhi ya wadau kama Jambao na wazazi katika kuendeleza mchezo huo.

Serikali inakiri kuwa riadha nchini inabebwa na mikoa hiyo kwa kiwango kikubwa hivyo inashirikiana na RT kuboresha miundombinu ili kuendeleza mchezo huo.

Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo, Yusuph Singo anasema kuna watu wanashirikiana nao kuboresha zaidi riadha mikoa hiyo na wakati wowote kuanzia sasa wataenda kuweka kambi kule kuweka mikakati ya kufanikisha jambo hilo.

“Mbali na mikoa hiyo, tunataka kuhakikisha riadha inachezwa mikoa yote na si Manyara na Singida pekee.

“Tumetenga shule 55 nchi nzima ambazo zitakuwa zikifundisha michezo ikiwamo riadha, lakini Manyara na Singida tutaipa kipaumbele katika hilo,” anasema Singo.