Rollers yaingiza mashabiki bure kuiona Yanga

Muktasari:

  • Klabu hiyo imetoa jumla ya tiketi 100 za bure kwa wanafunzi wa Shule ya Sir Seretse Khama CJSS ili waongeze hamasa kwenye mchezo huo

 Siku moja kabla ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Township Rollers, Yanga imesababisha mchecheto kwa wenyeji wao ambao wameonekana kuandaa lundo la mikakati ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri yatakayowavusha kwenda hatua inayofuata ya mashindano hayo.

Township Rollers wanahitaji ushindi au sare ya aina yoyote kwenye mchezo huo ili waingie hatua ya makundi kufuatia ushindi wa mabao 2-1 walioupata kwenye mchezo wa kwanza hapa Dar es Salaam, lakini wameonekana kuwa na mipango mingi kuelekea mechi ya marudiano inayoashiria wazi kwamba hawajiamini.

Katika kuhakikisha idadi kubwa ya mashabiki inajitokeza kuwaunga mkono nyumbani, timu hiyo imeanza kuuza tiketi za mechi hiyo tangu Jumatatu mwanzoni mwa wiki hii huku wakitumia mitandao yao ya kijamii kuhamasisha zaidi mashabiki kujitokeza uwanjani kesho.

"Ili ujihisi una umuhimu, nguvu, fahari na furaha katika mchezo kama mmoja wa mashabiki, Uwanja wa Taifa ndio sehemu unayopaswa kuwepo Jumamosi mchana. Nunua tiketi yako katika Makao Makuu ya Rollers au katika maduka yote ya  Liquorama, Gaborone," imeandika mitandao ya kijamii ya klabu hiyo.

Matangazo hayo yameonekana kuzaa matunda kwani hadi leo asubuhi, zaidi ya 65% ya tiketi za mchezo huo zilikuwa zimekwisha nunuliwa hali inayoonyesha kwamba huenda idadi kubwa ya mashabiki wakaujaza uwanja huo kesho.

Pia klabu hiyo imetoa jumla ya tiketi 100 za bure kwa wanafunzi wa Shule ya Sir Seretse Khama CJSS ili waongeze hamasa kwenye mchezo huo unaotarajiwa kufanyika saa 10.45 jioni kwa saa za Tanzania.