Ronaldo aanza tambo Juventus

Muktasari:

  • Alisema licha ya umri mkubwa wa miaka 33 anaamini ana nguvu ya kushindana ndio maana hakutaka kwenda kucheza soka Qatar au China kama wachezaji wa umri wake.

Turin, Italia. Mshambuliaji mpya wa Juventus ‘Kibibi Kizee’ cha Turin, Cristiano Ronaldo, ameahidi kuipa mataji likiwemo la Ligi ya Mabingwa Ulaya walilokosa tangu mwaka 1996.

Alisema licha ya umri mkubwa wa miaka 33 anaamini ana nguvu ya kushindana ndio maana hakutaka kwenda kucheza soka Qatar au China kama wachezaji wa umri wake.

“Ninafahamu kila klabu inatamani kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, nitahakikisha ninapambana kunyakuwa, sio hilo tu na mengine yote ikiwemo Ligi Kuu Italia ‘Serie A,” alisema.

Ronaldo aliahidi hayo juzi wakati wa utambulisho wake kwa mashabiki wa Juventus kwenye Uwanja wa Allianz mjini Turin, baada ya kufuzu vipimo vya afya.

Nahodha huyo wa Ureno aliyecheza kwa miaka tisa Real Madrid akiipa kila ubingwa, alisema atalipa fadhila kwa uongozi wa Juventus kumuamini na kumsajili.

Alisema hafikirii kuwa mfungaji bora wa muda wote Juventus kama alivyofanya Real Madrid alikofunga mabao 450, lakini atajitahidi kufunga mabao mengi yatakayowapa mataji.

“Mimi ni tofauti na wachezaji wengine wote ambao wanafikiri umri wao wa kucheza soka umemalizika, ninataka kuwaonyesha kuwa mimi ni tofauti na wao, najua kuwa ni jambo kubwa kwa kuwa nina miaka 33 na sio 23,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United aliyeibuliwa na kocha Sir Alex Ferguson kutoka Sporting Lisbon ya Ureno.