Ronaldo apiga bao mia Real

Muktasari:

  • Ronaldo ndiye mshambuliaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa

Madrid, Hispania. Mshambuliaji nyota Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameweka rekodi mpya ya mabao katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa UIaya.

Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufikisha mabao 100 akiwa na klabu moja.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ureno, juzi usiku alifunga mabao mawili Real Madrid iliposhinda mabao 3-1 dhidi ya Paris Saint Germain PSG katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Beki wa kushoto Marcelo, alifunga bao la tatu kwa mkwaju mkali na kuwapa raha mashabiki wa klabu hiyo waliomiminika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, Hispania.

Hakuna mchezaji aliyewahi kufikisha idadi ya mabao 100 akicheza katika klabu moja kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Nguli huyo amefikisha mabao 101 katika mashindano hayo. Bao la PSG lilifungwa na Adrien Rabiot.

Lionel Messi wa Barcelona anashika nafasi ya pili katika mashindano hayo baada ya kufikisha mabao 97.

Nahodha huyo wa Argentina anashika nafasi ya pili akifuatiwa na nyota wa zamani wa Real Madrid Raul Gonzalez.

Raul, aliyekuwa nahodha wa Real Madrid, alifunga mabao 66 katika miaka 21 aliyocheza Santiago Bernabeu. Alessandro Del Piero anafuatia kwa mabao 42 akiwa na kikosi cha Juventus.