Nne zafuzu nusu fainali Rwakatare Cup

Muktasari:

Bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia Sh2milioni

Morogoro. Mabingwa wa soka mkoa wa Morogoro msimu wa 2017/2018, Shupavu FC imeshindwa kutinga nusu fainali ya Rwakatare Cup 2017 baada ya kufungwa kwa penalti 5-3 na Idete FC.

Shupavu FC ilikumbana na kipigo hicho wakati wa mchezo mkali wa robo fainali uliopigwa jana kwenye Uwanja wa shule ya msingi Lukolongo kijiji cha Mngeta wilaya ya Kilombero mkoani hapa.

Katika mchezo huo war obo fainali ulishudia timu hizo zikimaliza dakika 90 bila ya kufungana ndipo penalti zilipotumika kuamua mshindi.

Kipa wa Idete FC, Mohamed Ngozi alikuwa kikwazo kwa Shupavu FC baada ya kuokoa penalty mbili na kuisaidia timu yake kushinda  kwa penalty 5-3.

Msimamizi mkuu wa Rwakatare Cup 2017, Supertus Duma alisema mbali ya Idete FC timu nyingine zilizofuzu kwa nusu fainali ni JKT Chita FC,  Melela Express na Super Mahakama FC.

JKT Chita FC ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mngeta Rangers FC, wakati Melela Express FC imesonga mbele kwa kuilaza City Boys FC 2-1, huku Super Mahakama FC ilitinga nusu fainali bila jasho baada ya Teachers FC ya Mlimba kushindwa kutokea uwanjani.

 “Nusu fainali ya kwanza Rwakatare Cup 2017 itawakutanisha Super Mahakama FC dhidi ya JKT Chita FC leo (Jumanne) na nusu fainali ya pili itakuwa kati ya Melela Express FC na Idete FC (kesho Jumatano),” alisema Duma.

Duma alisema fainali itachezwa Ijumaa Novemba 24 na bingwa  atakabidhiwa zawadi ya fedha taslimu Sh2 milioni wakati mshindi wa pili atapata Sh1milioni.