Zidane amtaka Salah

Muktasari:

Mshambuliaji huyo wa Misri amekuwa katika kiwango cha juu msimu huu

Madrid, Hispania. Zinedine Zidane amezungumzia kuhusu uwezekano wa Real Madrid kumsajilia Mohamed Salah baada ya kukiri aina ya uchezaji wa nyota huyo wa Liverpool nimvutia sana.

Salah kwa sasa ndiye anayeongoza katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu England akiwa na mabao 13, akiwa ndiyo kwanza miezi sita tangu amejiunga na Liverpool akitokea Roma.

Hata hivyo anauzoefu wa soka la England kwani alishawahi kucheza Chelsea japokuwa hakuwa na wakati mzuri, lakini kasi yake ya sasa ndani ya Liverpool inawapa shaka mashabiki wa klabu hiyo kwamba Mmisri huyo uenda akatakiwa na klabu nyingine kubwa.

Real Madrid kwa sasa inatafuta mshambuliaji mpya, na Salah amekuwa akihusishwa na kutaka kujiunga na Real.

Kocha wake wa timu ya taifa ya Misri, Hector Cuper alidai Real ipo katika hatua za mwisho kumfuata nyota huyo.

Wakati mshambuliaji wa zamani wa Misri, Mido alidai anaamini Salah hataaminia Santiago Bernabeu wakati wowote kuanzia sasa.

Na Zidane mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kumsajili Salah ambaye kiwango chake cha sasa kimekuwa cha hali ya juu sana.

Zizou alisema: “Salah ni mchezaji bora. Ameonyesha hivyo akiwa Roma, na sasa Liverpool.

 “Bado ni kijana amekuwa akibadilika kila siku. Sipendi sana kuzungumzia wachezaji nje ya timu yangu, lakini yeye ni mchezaji anayenivutia sana.”

Eden Hazard pia amekuwa akihusishwa na kutaka kujiunga na  Real msimu ujao, lakini Zidane akili yake kwa sasa ipo kwa Salah.