Sanga, Takukuru wafunguka fedha za Yanga

Muktasari:

  • Jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii kulizuka taarifa zilizodai kuwa baadhi ya viongozi wa Yanga walihusika na ubadhirifu wa fedha zilizotajwa kufikia Sh440 milioni na taarifa hizo zilikwenda mbele zaidi na kudai kwamba pesa hizo zilizochotwa kwa kipindi cha miezi miwili pekee iliyopita.

Dar es Salaam. Wakati Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Nchini (Takukuru), ikisema haina taarifa za ubadhirifu wa fedha ndani ya Yanga, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga ameanika ukweli kuhusu tuhuma hizo.

Jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii kulizuka taarifa zilizodai kuwa baadhi ya viongozi wa Yanga walihusika na ubadhirifu wa fedha zilizotajwa kufikia Sh440 milioni na taarifa hizo zilikwenda mbele zaidi na kudai kwamba pesa hizo zilizochotwa kwa kipindi cha miezi miwili pekee iliyopita.

Fedha zinazodaiwa kuchotwa ni Sh240 milioni zikiwa ni malipo ya awali kutoka Kampuni ya SportsPesa na Sh200 milioni sehemu ya mgawo kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Hata hivyo Sanga alikanusha vikali akisema taarifa hizo zina lengo la kuibua machafuko na ametoa rai kwa wanachama wa klabu hiyo kutulia kwa kuwa Yanga inapitia kipindi kigumu.

Sanga alisema kuwa hakuna kiongozi wa Yanga aliyetafuna fedha hizo kama taarifa hizo zinavyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Taarifa zilizozagaa jana kwenye mitandao zilidai suala hilo limepelekwa Takukuru kwa uchunguzi na waliohusika wajiandae kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa Takukuru, Musa Misalaba alisema kuwa hana taarifa hiyo ingawa alikiri kuwepo kesi nyingi za Simba na Yanga ofisini kwao.

“Hizi Simba na Yanga zina kesi nyingi tu huku kwetu, lakini hiyo ya ubadhirifu wa milioni 440 sina taarifa zake,” alisema Misalaba.

“Yanga sasa hivi iko katika kipindi kigumu kiuchumi, kweli mtu anaweza kuchukua fedha hizo? Walishindwa kuiba enzi zile Yanga iko peponi miaka mitano iliyopita inakwenda kuweka kambi Uturuki iwe sasa ambapo timu ina hali mbaya kiuchumi?,” alihoji Sanga na kuendelea.

“Timu imekwenda kucheza Kenya na Gor Mahia, watu wametumia fedha zao za mifukoni kutokana na mapenzi, leo hii mtu anaandika kwenye mtandao vitu visivyokuwa na ukweli.

“Sawa tunapata udhamini wa Azam ni milioni 300 kwa mwaka ambayo kwa matumizi ya Yanga ni fedha ya matumizi ya miezi miwili tu imekwisha, hiyo miezi mingine 10 tunajiendeshaje?

“Tunakatwa asilimia 55 kwenye mapato yetu kwa ajili ya kodi ya ardhi, timu ilifikia mahali tukapata mgawo wa shilingi laki moja kwenye mechi na Mwadui, lakini bado tumeweza kuifikisha hatua ya makundi kimataifa, bado kuna watu hawalioni hilo,” alisema Sanga.

Pia Sanga alisema atakuwa tayari kujiuzulu wadhifa wake, lakini hawezi kuchukua uamuzi huo kwa kuwa hakuna mtu wa kumkabidhi klabu.

“Naweza kumuandikia barua Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini kama wengine walivyoamua kuandika barua, lakini nitakuwa nafanya kinyume na Katiba ya Yanga, (George) Mkuchika ataiendeshaje? tutakuwa hatujengi zaidi ya kubomoa,” alisema Sanga.

Makamu Mwenyekiti huyo alidai fedha wanazopata kwenye udhamini zinaonekana nyingi kwa mtazamo wa baadhi ya watu alizodai hazitoshi kwa uendeshaji wa shughuli za klabu.

“Yusuf (Manji) aliamua kubadili mfumo, akataka aikodishe Yanga wakasema hatumtaki, tulimtegemea sana katika kutoa fedha, sasa timu haina fedha hakuna anayejitokeza kusaidia, lakini wanakuwa wa kwanza kueleza upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii.

Manji/Mkutano

Sanga alisema hawezi kuitisha mkutano mkuu wa dharura kwa kuwa sio muda mwafaka kutokana na mazingira ndani ya klabu.

“Kuna watu wanahamasisha vurugu kwenye mitandao ya kijamii, sidhani kama tunajenga Yanga, kama kuna jambo ni vizuri tukae mezani tujue nini cha kufanya tupate mwafaka,” alisema Sanga.

Kuhusu kurejea mwenyekiti wao wa zamani, mfanyabiashara Yusufu Manji, Sanga alidai itakuwa ngumu kwa sasa kwani mazingira ndani ya klabu si rafiki kwa mtu kuwekeza.

Wachezaji roho kwatu

Wachezaji wa Yanga jana walitoka kwenye mkutano wakiwa na nyuso za tabasamu zilizoashiria kwamba wameridhika na ahadi za viongozi wao.

Jana Jumapili uongozi wa Yanga ulifanya kikao na wachezaji 19 Makao Makuu Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam kuanzia saa sita mchana na kumalizika 9:25 alasiri.

Vigogo wa Yanga waliohudhuria ni Hussen Nyika, Mustapha Olungo, Hussen Ndama, Mussa Katabalo, Mzee Mashauri na Hafidhi Saleh ambaye ni maneja.

Wachezaji walioudhuria ni Yuothe Rostand, Ramadhani Kabwili, Hassani Kessy, Said Makapu, Raphael Daud, Pius Buswita, Yusuph Mhilu, Said Mussa, Yohana Mkomola, Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Amiss Tambwe.

Wengine ni Thabani Kamusoko, Papy Tshishimbi, Baruan Akilimali, Godfrey Mwashuiya, Patho Ngonyani, Juma Abdul na Nadir Haroub ‘Cannavarro’.

“Tumekubaliana kuwalipa wachezaji kile ambacho wanadai kabla ya ligi kuanza, hilo ndilo lilikuwa kubwa na likatufanya tukae kikao kirefu na kizito.

“Tutawapa wanaodai mishahara, posho zao zote, pesa zilizobaki katika usajili na kila stahiki ya mchezaji atapata kwa wakati mambo yote yanakwenda vizuri kama tulivyokubaliana.

“Wachezaji walisema walipoteza mechi na Gor Mahia kwa kuwa hawakuwa vizuri kisaikolojia, lakini kwa kuwa wana uhakika wa kupata stahiki zao kwa wakati kesho (leo) Jumatatu watakuwa wote mazoezini,” alisema mmoja wa vigogo.

Meneja wa Yanga, Saleh alisema kikao kilikuwa na manufaa na wamekubaliana kuanza maandalizi ya kujiandaa na mechi za kimataifa ukiwemo mchezo dhidi ya Gor Mahia.