Sarri ampigia hesabu Elseid Hysaj

Muktasari:

  • Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri ambaye amekuwa na mwanzo mzuri, amepanga kukiimarisha zaidi kikosi chake kwa kumsajili beki wa pembeni kulia chipukizi kutoka nchini Albania anayekipiga Napoli, Elseid Hysaj.

London, England. Kocha wa timu ya Chelsea, Maurizio Sarri, amejipambanua kuwa ni mmoja wa makocha bora duniani, baada ya kuleta mapinduzi ya haraka, amepanga kuanza kuimarisha kikosi chake.

Sarri aliyetua Stamford Bridge, wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi akitokea Napoli ya Italia, alitumia muda mchache kukijenga kikosi akiwatumia wachezaji wale wale aliowakuta na kuongeza wachache.

Wachezaji aliowanunua Sarri baada ya kutua Chelsea ni makipa wawili, Kepa Arrizabalaga na Rob Green, na viungo Mateo Kovavic raia wa Croatia na Jorignho raia wa Brazil.

Katika dirisha la usajili la Januari Sarri amepanga kuongeza vifaa vingine na moja ya wachezaji ambao anata kuwasajili ni mlinzi wa pembeni kulia aliyemnoa katika kikosi Napoli, Elseid Hysaj raia wa Albania.

Sarri anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na bodi ya Chelsea akiwemo Mtendaji Mkuu Marina Granovskaia pamoja na mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich.

Kocha huyo raia wa Italia, amekuwa mkimya sana kuzungumzia usajili na pia ameonekana kujua kubana matumizi asiyependa kugombea kwani kati ya wachezaji wanne aliowasajili klabuni hapo wawili aliwasajiliwa kwa dau dogo kwa kuwa walikuwa wachezaji huru.