Serengeti Boys haikamatiki

Muktasari:

  • Katika orodha hiyo, straika wa Uganda, Ssekajja David ndiye kinara akifunga mabao manne akiwa mchezaji wa kwanza kutupia hat trick katika mashindano hayo kabla ya Mkenya, Richdonald Steward kumjibu wikiendi iliyopita.

VIJANA wanatupia bwana! Unaambiwa kabla ya mechi za jana Jumapili katika michuano ya kuzufu fainali za AFCON-2019 kwa Vijana U17 jumla ya mabao 53 yametupiwa kambani na wachezaji 18 likiwamo moja la kujifunga.
Katika orodha hiyo, straika wa Uganda, Ssekajja David ndiye kinara akifunga mabao manne akiwa mchezaji wa kwanza kutupia hat trick katika mashindano hayo kabla ya Mkenya, Richdonald Steward kumjibu wikiendi iliyopita.
Nyota sita, wakiwamo Watanzania, Kelvin John 'Mbappe' na Akiri Ngoda ndio wanaomfukuzia Mganda huyo nyuma yake kwa kila mmoja kufunga mabao matatu, huku wachezaji saba wengine wakifuatia kila mmoja akifunga mabao mawilimawili.
Katika wachezaji waliotupia bao moja moja wavuni idadi yao ipo 17, akiwamo kipa Omer Yousif wa Sudan  aliyejifunga wakati akijaribu kuokoa kona ya timu ya Tanzania siku timu yao ilipofumuliwa mabao 5-0 na Serengeti Boys.
Mpaka sasa safau ya ushambuliaji ya Kenya ndio imeonekana tishio kwa kutupia kambani mabao 13 katika mechi mbili tu (kabla ya mchezo wao wa jana), ikifuatiwa na Burundi yenye mabao nane kutokana na mechi tatu na Tanzania na Rwanda zikifuatia kwa kutupia kila moja mara saba ikiitangulia Uganda yenye mabao sita.
Kwa timu yenye ukuta mwepesi, Djibouti ndio kinara ikiruhusu mabao 15 katika mechi zao tatu, ikifuatiwa na timu za Sudana  (12) na Sudan Kusini (11), huku timu ngumu kufungika zikiwa ni Kenya na Ethiopia ambazo haijaruhusu bao lolote.