Serengeti Boys kulinda heshima dhidi ya Rwanda leo

Muktasari:

  • Mchezo huo wa Kundi A utakaoanza saa 11:00 jioni, utakuwa wa kukamilisha ratiba kwani timu zote zimeshaingia nusu fainali ya michuano hiyo kutoka kundi hilo.

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, na Rwanda leo jioni zitashuka dimbani katika mechi ya mwisho kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo kutoka Kanda ya Cecafa.

Mchezo huo wa Kundi A utakaoanza saa 11:00 jioni, utakuwa wa kukamilisha ratiba kwani timu zote zimeshaingia nusu fainali ya michuano hiyo kutoka kundi hilo.

Kuingia hatua hiyo, Serengeti Boys iliifunga Burundi mabao 2-1 kabla ya kuizabua Sudan mabao 5-0

Serengeti Boys ilishinda mechi zake zote mbili za kwanza ikiichapa Burundi na Sudan sawa na Rwanda na zote zimefuzu hatua na nusu fainali na leo zitasaka mshindi wa kwanza wa kundi lao.

Kuingia hatua hiyo, Rwanda iliifunga Burundi 4-3 pamoja na Sudan mabao 3-1. Timu hizo zinalingana kwa kila kitu isipokuwa zinatofautiana mabao ya kufungwa. Tanzania imefungwa bao moja wakati Rwanda imefungwa manne.

Hata hivyo, mchezo huo unaweza kuwa mkali ama wa kawaida kwa kuwa hakuna timu itakayokuwa na cha kupoteza kwa kuwa zimeshakata tiketi na kilichopo ni mechi za kulinda heshima.

Timu nyingine kutoka Kundi B ukiondoa Ethiopia yenye pointi tisa zitakuwa zikiwania nafasi hiyo kati ya Kenya na Uganda kuhitimisha mechi zao kwa kuwa kila mmoja ana pointi sita.

Kenya na Ethiopia zinacheza kesho wakati Uganda itakwaana na Djibouti.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo alisema kuwa hawatawaachia Rwanda na anachotaka ni kuhakikisha wanawapiga.

“Sisi tumeingia kwenye mashindano na kila atakayekuwa mbele yetu tutampiga tu, hatutaangalia wa kumkimbia au kumkwepa, kila tutakayekutana naye tutapambana naye na tutashinda,” alisema Milambo.

Alisema wachezaji wake wako sawasawa tayari kwa mchezo huo ambao watahakikisha wanashinda ili kutengeneza kujiamini katika mashindano hayo na yanayokuja mbele yao.