Simba, Azam uso kwa uso fainali Kombe la Kagame, Kagere ang’ara

Muktasari:

  • Azam ilitangulia kufuzu fainali baada ya kuilaza Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 katika mchezo wa awali wa nusu fainali uliochezwa dakika 120.

Mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame Azam, watacheza mchezo wa fainali na Simba Jumapili wiki hii, baada ya timu hizo kushinda mechi zao za leo Jumatano.

Azam ilitangulia kufuzu fainali baada ya kuilaza Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 katika mchezo wa awali wa nusu fainali uliochezwa dakika 120.

Mabao ya Azam katika mechi hiyo yalifungwa na mshambuliaji mpya Ditram Nchimbi dakika ya 91 kwa kiki kali kabla ya Bruce Kangwa kufunga la pili dakika ya 99.

Simba ilipata ushindi wake kwa mbinde baada ya kuichapa JKU ya Zanzibar bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali ya pili. Mechi zote zilichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nyota ya mshambuliaji mpya wa Simba, Meddie Kagere, iliendelea kung’ara, baada ya jana kufunga bao pekee dakika ya 44.

Shambulio la bao hilo lilianzia katikati mwa uwanja baada ya Mzamiru Yassin kumpoka mpira Faisal Salum na kumpa pasi Nicholaus Gyan aliyefanya kazi ya ziada kuwatoka wachezaji watatu wa JKU kabla ya kupenyeza mpira kwa Kagere aliyefunga kwa shuti la mguu wa kulia.

Bao liliibua malalamiko kutoka kwa wachezaji JKU ambao walimzonga kwa muda mwamuzi wa mechi hiyo, Omar Abdulkadir kutoka Somalia wakidai Faisal alichezewa madhambi kabla ya kupokwa mpira.

Tofauti na matarajio ya wengi kuwa Simba ingepata mteremko kwenye mchezo huo, mambo hayakuwa mepesi kutokana na mbinu ambazo wapinzani wao walitumia kuanzia mwanzoni mwa mchezo.

JKU ilianza kucheza soka la mabavu lililoambatana na rafu za mara kwa mara ikionekana ni mbinu ya kuwatoa mchezoni wachezaji wa Simba ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mashindano hayo.