Simba, Yanga, zapangua, kikosi, Azam, FC

Muktasari:

  • Azam imeamua kufanya usajili wa nguvu ukiwa na lengo la kushindana na Simba, Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Dar es Salaam. Klabu ya Azam inahaha kuziba mapengo ya wachezaji wanane muhimu ambao tangu kuondoka kwao, timu hiyo imeshindwa kufua dafu mbele ya Simba na Yanga ambazo zimetawala kwa misimu mitatu mfululizo.

Azam imeamua kufanya usajili wa nguvu ukiwa na lengo la kushindana na Simba, Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Tangu Azam ilipotwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) mwaka 2015, imeshindwa kuwa na makali ya kupambana na klabu hizo kongwe nchini ambazo zimekuwa zikibadilishana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.

Mafanikio ya kutwaa Kombe la Kagame yalikuwa ni hitimisho la ‘Kizazi cha Dhahabu’ cha Azam ambacho kabla ya hapo kilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu 2013/2014 bila kupoteza mchezo.

Kikosi hicho cha dhahabu kiliundwa na Aishi Manula, Himid Mao, Said Morad, Aggrey Morris, Paschal Wawa, Erasto Nyoni, Baptiste Mugiraneza, Farid Musa, Kipre Tcheche, John Bocco na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Baada ya kupata mafanikio hayo, mastaa wanane waliondoka Azam kwa nyakati tofauti na kuifanya timu hiyo kuyumba katika misimu iliyofuata 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018 uliomalizika mwezi uliopita.

Nuksi kwa Azam ilianza baada ya kuondoka Morad ambaye aliunda safu imara ya ulinzi akicheza pacha na Aggrey Morris, Wawa katika mfumo wa 3-5-2 uliokuwa ukipendelewa kutumiwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Stewart Hall.

Mwaka mmoja uliofuata baada ya Morad kuondoka Azam, timu hiyo ilijikuta ikiwapoteza nyota wanne waliokuwa nguzo muhimu Farid, Tcheche, Mugiraneza na Wawa.

Wakati Farid akiondoka na kujiunga na CD Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania, Tcheche alitimkia Al Nahda iliyopo Ligi Kuu Oman na Mugiraneza alitua Gor Mahia ingawa hakudumu muda mrefu.

Wakati ikionja machungu ya kuwapoteza Morad, Wawa, Kipre, Mugiraneza na Farid, mwaka 2017 ulikuwa mbaya baada ya kuwapoteza Nyoni, Bocco na Kapombe waliotimkia Simba.

Kuondoka kwa nyota hao watatu na Manula kulielezwa kama utekelezaji wa mpango wa klabu hiyo kupunguza matumizi ingawa pengo la Manula aliyekuwepo kwenye ‘Kizazi cha Dhahabu’ halijaonekana kuiathiri Azam kutokana na uwepo wa makipa Mwadini Ally na Razack Abarola wanaofanya vizuri.

Ikionekana kama inajifunza kutokana na makosa, Azam imekuwa na mikakati imara ya kuimarisha benchi lake la ufundi na kufanya usajili wa nyota mbalimbali walioonyesha kiwango bora wakiamini inaweza kuwa mwanzo wa kutengeneza kizazi kingine cha dhahabu.

Azam imeimarisha benchi la ufundi kwa kumchukua kocha Hans van der Pluijm na aliyekuwa msaidizi wake Yanga, Juma Mwambusi atakayeungana na Idd Cheche kumsaidia kocha huyo wa zamani wa Singida United.

Kwa upande wa usajili imewanasa mshambuliaji Donald Ngoma, Ditram Nchimbi, Tafadzwa Kutinyu na Nico ‘Wakiro’ Wadada.

Azam ina takribani nyota saba wanaocheza safu ya ushambuliaji Waziri Junior, Mbaraka Yusuph, Yahya Zayd, Shabani Iddi, Paul Peter Ngoma na Nchimbi.

Kocha msaidizi wa Azam, Cheche alisema timu yake inasajili kwa kuangalia mahitaji na sio kushindana na Simba au Yanga.

“Unajua hadi sasa sera ya Azam haijulikani hasa ni ipi kwa sababu msimu uliopita walisema wanataka kuwapa nafasi vijana lakini ghafla wamebadilika na wamerudi kulekule walikotoka.

“Usajili na mabadiliko haya ya benchi waliyofanya sidhani kama yanaweza kuifanya iwe na kikosi bora cha muda mrefu. Kwa mtazamo wangu naona Azam inataka mafanikio kwa muda mfupi,”alisema kocha Joseph Kanakamfumu.