Simba SC haitanii kabisa

Muktasari:

  • Simba imeirarua bila huruma Njombe Mji mabao 4-0 na sasa inaisubiri Yanga Jumamosi ijayo.

 Unaweza kusema, Simba hawatanii. Wameamua msimu huu kutawazwa ubingwa baada ya miaka mitano ya kuukosa.

Simba imerudia makali yake iliyoanza nayo kwa kuirarua Njombe Mji mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ikimkaribisha kocha msaidizi mpya Mrundi Masudi Djuma ambaye ni mbadala wa Jackosn Mayanja, imefikisha pointi 15 huku ikiwa na mabao 19, ikiwa kileleni.

Ushindi wa Simba unaweza kuwa na maana mbili, kwanza kujikita kileleni mwa msimamo, lakini pia ni salamu kwa mahasimu wao Yanga, wanaokutana nao mchezo unaofuata.

Yanga yenyewe iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 12 na leo inacheza na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage.

Endapo Yanga itapoteza mchezo huo au kupata sare itatoa fursa kwa Simba kukaa patamu zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu inayoshirikisha timu 16 za Tanzania Bara.

Mchezo wenyewe sasa

Simba ilicheza kandanda murua huku safu ya kiungo ikiwa chachu ya ushindi huo.

Ikishuhudiwa na Masudi aliyekuwa jukwaani kwa kuwa hakuwa na kibali cha kufanya kazi nchini kwa mujibu wa sheria za nchi, alionekana akifuatilia kwa makini mchezo huo na muda mrefu alionekana mwenye hisia na wakati mwingine alitumia muda mrefu akiwa amejishika tama.

Katika mchezo wa jana, muungano mzuri wa safu ya kiungo ilikuwa siri ya ushindi kwa Simba jana.

Njombe Mji imebakiwa na pointi tano na inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Baada ya kusugua benchi muda mrefu, nahodha wa zamani wa timu hiyo Jonas Mkude, alicheza vyema katika nafasi ya kiungo mkabaji (namba sita), akicheza pacha na Haruna Niyonzima na Mzamiru Yassin.

Mkude, Niyonzima na Mzamiru walitawala dimba la kati na kuwapa wakati mgumu mabeki wa Njombe Mji ambao walielekeza nguvu nyingi kwa Okwi na kusahau wengine.

Mzamiru aliyekuwa akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji alifunga mabao mawili baada ya kuongeza juhudi kipindi cha kwanza tofauti na dakika 45 za mwanzo ambapo alionekana amepwaya.

Njombe Mji inayonolewa na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mrage Kabange, itajilaumu kwa mchezo wa kupaki basi tangu mwanzo wa mchezo hatua iliyowapa nafasi kina Mkude kuongeza kasi ya mashambulizi.

Kwa takribani dakika 15 za mwanzo, Njombe Mji iliyopanda Ligi Kuu na timu za Lipuli Iringa, Singida United ilicheza kwa kujihami ikiwa na dhamira ya kutaka pointi moja.

Baada ya Simba kubaini janja hiyo ilianza kuwavuta kwa mashambulizi ya pembeni kutoka kwa mabeki wa kulia Erasto Nyoni na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Nyoni alikuwa mwiba kwa mabeki wa Njombe Mji kwa kuwa alikuwa akipanda mbele kupiga mipira ya krosi na moja ya shuti lake lilizaa matunda. Pia Tshabalala aliyerejea uwanjani kwa kishindo akitokea katika maumivu yaliyomuweka nje ya uwanja muda mrefu.

Mabao mawili ya Mzamiru Yassin na mawili ya Emmanuel Okwi na Laudit Mavugo yalitosha kuifanya Simba izidi kutakata kileleni na hivyo kuongeza presha kubwa kwa Yanga ambayo inaikabili Stand United leo ugenini kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

Okwi alifungua karamu ya mabao kwa kuipatia Simba bao la kwanza dakika ya 28 kwa mpira wa kichwa uliogonga mwamba wa pembeni na kutinga wavuni akimalizia krosi ya Nyoni.

Bao la pili lilipatikana dakika ya 51 lililofungwa na Mzamiru kwa shuti kali akimaliza pasi ya Niyonzima kabla ya kufunga la tatu dakika ya 52 kutokana na kazi nzuri ya Okwi.

Simba iliongeza bao la nne dakika ya 58 lililofungwa na Laudit Mavugo kwa kichwa baada ya krosi ya Shiza Kichuya.

Awali, mpira ulianza taratibu huku timu zote zikisomana lakini dakika ya nane Njombe Mji ilipata mpira wa kona uliopigwa na Awadh Salum, lakini haikuzaa matunda.

Mfumo wa kupaki basi uliipa wakati mgumu Simba kupenya ngome ya Njombe Mji kwa takribani dakika 25 kipindi cha kwanza licha ya kulishambulia kwa nguvu lango la wapinzani wao.

Katika mchezo huo Simba ilimtoa Mavugo, Niyonzima, Mzamiru na kuingia Nicholaus Gyan, Mohammed Ibrahim ‘MO’ na Said Ndemla. Njombe Mji iliwatoa Innocent Lazaro, David Kissu na kuingia Christopher Kasewa na Rajabu Mbululo.

Vikosi

Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein, Juuko Musrhid, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.

Njombe: David Kissu, Agaton Mapunda, Innocent Lazaro, Ahmed Adiwale, Laban Kambole, Joshua John, Awadh Salum, Jimmy Mwaisondela, Adam Bako, Ditram Nchimbi na Claide Wingenge.