Singida United yajipanga upya

Muktasari:

Singida Utd kwa sasa ipo nafasi ya nne ikiwa inapambana kuvunja rekodi ya Mbeya City ambayo msimu wake wa kwanza ilimaliza nafasi ya tatu

Mwanza. Kocha wa Singida United, Hans Pluijm amesema kikosi chake kinahitaji kujituma zaidi katika mzunguko huu ili kumaliza katika nafasi tatu za juu

Singida United ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo uliopigwa jana Jumatano kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ushindi huo umeifanya Singida United kufikisha pointi 33 ikiwa katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ambapo Simba inaongoza ikiwa kwa pointi 41.

Kocha Pluijm alisema Ligi Kuu sasa ni ngumu hivyo amewaambia wachezaji wangu ni lazima wapambane kweli kweli kama wanataka kupata matokeo mazuri katika mechi zilizobaki.

Akizungumzia mechi yake dhidi ya Mbao FC, kocha huyo alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kwao haswa kipindi cha kwanza, lakini ameshukuru kupata pointi tatu.

“Ndio maana nasema ligi imekuwa ngumu kupata ushindi unatakiwa kupambana vilivyo ndani ya dakika 90 huu mchezo wetu wenzatu walitubana sana kipindi cha kwanza,” alisema Pluijm.

Nahodha wa timu hiyo, Mudathiri Yahaya alikiri ugumu wa Ligi Kuu wamejipanga kuhakikisha kila mechi wanapata matokeo mazuri.