Simba kileleni, Yanga kibaruani

Sunday November 19 2017

 

By Waandishi Wetu,Mwananchi [email protected]

Timu ya Simba imeondoa nuksi ya miaka minne na miezi tisa ya kushindwa kupata ushindi mbele ya Prisons inapocheza kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mara ya mwisho Prisons ilifungwa bao 1-0 na Simba katika mchezo uliochezwa Februari 13,2013.

Lakini jana alikuwa ni John Bocco aliyeondoa nuksi hiyo kwa kufunga bao pekee katika mchezo huo, hilo likiwa ni bao lake la pili msimu huu.

Nahodha huyo wa zamani wa Azam, alifunga bao hilo kwa shuti la mguu wa kulia katika dakika ya 84, baada ya kugeuka kwa kasi kuuwahi mpira uliokolewa vibaya na mabeki na kuachia mkwaju mkali.

Wakati Bocco akifunga bao hilo, baadhi ya mashabiki wa Simba walikuwa wameshaanza kutoka nje kwa kukata tamaa wakiamini timu hizo zitatoka suhulu.

Simba imezidi kuikimbia Yanga baada ya kufikisha pointi 22, pointi tano mbele ya mabingwa hao watetezi wanaoshuka dimbani leo kuikabili Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Bocco alisema anaona fahari kufunga bao muhimu lililowapa pointi tatu na wametimiza malengo ya kuondoka na pointi sita katika michezo yote miwili mkoa wa Mbeya.

“Tulimiliki mpira kipindi cha kwanza, lakini hatukufunga. Wakati wa mapumziko kocha alituambia tutulie na tukafanya hivyo kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao,” alisema Bocco.

Naye mshambuliaji wa Prisons, Mohammed Rashid aliwatupia lawama mabeki wa timu hiyo akidai ndio chanzo cha kufungwa.

“Ukweli tumecheza vizuri muda wote lakini makosa yametugharimu. Tumefungwa kutokana na makosa ya mabeki na Bocco akatumia nafasi vizuri,” alisema Rashid anayewindwa kwa nguvu na klabu za Yanga na Simba katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 15 hadi Desemba 15.

Mchezo ulivyokuwa

Timu zote zilianza kwa kushambulina kwa zamu, lakini mabeki wa timu hizo walikuwa imara kuondoa hatari.

Dakika ya 35 Shiza Kichuya wa Simba alikosa bao akiwa mbele ya lango, baada ya kugongeana vizuri na Mwinyi Kazimoto na Bocco.

Dakika ya 35 Kichuya aliambaa tena na mpira lakini aliachia shuti kali lililopaa kabla ya Prisons kujibu shambulizi hilo dakika ya 38 kupitia kwa Rashid aliyemjaribu kipa Aishi Manula kwa shuti alilodaka.

Simba ilifanya mabadiliko iliwatoa Haruna Niyonzima na Mwinyi Kazimoto na nafasi zao kuchukuliwa na Mohammed Ibrahim na Laudit Mavugo.

Kwenye Uwanja wa Mabatini, kibonde Ruvu Shooting imeona mwezi baada ya kuichapa Ndanda bao 1-0, lililofungwa na Abdulrahman Musa.

Uwanja wa Majimaji Songea, wenyeji Majimaji waliifunga Mbao mabao 2-1 wakati Kambarage Shinyanga, Stand United ilitoka suluhu na watani wao wa jadi Mwadui.

Yanga kuivaa Mbeya City

Yanga itaikabili Mbeya City leo ikiwa na idadi kubwa ya wachezaji majeruhi, hivyo kocha George Lwandamina anatakiwa kujipanga kikamilifu ili kupata ushindi katika mchezo huo.

Yanga inatarajiwa kuwakosa Pappy Shitshimbi, Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao ni majeruhi.

Mbeya City ambayo mchezo uliopita ilichapwa bao 1-0 na Simba jijini Mbeya, leo imepania kusahihisha makosa na kupata ushindi mbele ya Yanga.

Yanga inajivunia rekodi bora dhidi ya Mbeya City ikicheza Dar es Salaam. Timu hiyo imeshinda mechi zote nne zilipovaana.

Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa’Fusso’ alisema ingawa wana majeruhi wengi, lakini watapambana kupata ushindi katika mchezo huo ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.

Kocha msaidizi wa Mbeya City, Mohammed Kijuso alisema wamepanga kumaliza rekodi mbaya dhidi ya Yanga kwa kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza dhidi ya mabingwa hao watetezi.

Oliver Albert (Dar), Godfrey Kahango (Mbeya) na Masoud Masasi, Shinyanga.

Advertisement