Friday, November 3, 2017

Simba waifuata Mbeya City kwa ndege

 

Vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba mchana wa leo wanatarajia kupanda pipa kuelekea Mbeya kuwahi pambano lao dhidi ya Mbeya City litakalopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini humo.

Timu hiyo itaondoka jijini Dar es Salaam saa 6 mchana kwa usafiri wa ndege.

Mratibu wa Simba, Ally Abbas alisema kikosi chao kilichokuwa kikifanya mazoezi tangu Jumatatu kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini kipo freshi vijana wote wakiwa hawana tatizo ukiondoa majeruhi wa awali wanaoendelea vema.

Simba inayoongoza msimamo kwa uwiano wa mabao ikiwazidi Yanga, Mtibwa Sugar na Azam wanaolingana nao kila moja akiwa na alama 16, itaenda kucheza na Mbeya City ikiwa na kumbukumbu ya sare ya 1-1 iliyopata kwa Yanga.

Pia ina kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa mwisho jijini humo dhidi ya Prisons katika ligi ya msimu uliopita.

Hata hivyo mabosi ya Mbeya kupitia Kocha Msaidizi wao, Mohammed Kijuso wametamba kuwa Simba wajipange kwani City isingependa kupoteza tena ikiwa nyumbani baada ya mechi yao iliyopita kulala 1-0 ugenini mbele ya Azam.

-->