Simba ni kufa au kupona Kombe la Mapinduzi leo

Muktasari:

  • Simba inahitaji angalau matokeo ya sare ili kuweza kutinga hatua ya nusu fainali lakini kama inataka kuongoza Kundi A ni lazima ihakikishe inaondoka na pointi zote tatu katika mchezo huo.

Zanzibar. Vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba leo Jumapili watazichanga karata zao za mwisho katika mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Jang’ombe Boys ya visiwani hapa mchezo utakaochezwa majira ya saa 10 jioni.

Simba inahitaji angalau matokeo ya sare ili kuweza kutinga hatua ya nusu fainali lakini kama inataka kuongoza Kundi A ni lazima ihakikishe inaondoka na pointi zote tatu katika mchezo huo.

Kundi A limekuwa na ushindani mkubwa ambapo Simba ndiyo vinara wakiwa na pointi saba na wanafuatiwa na Jang’ombe Boys na Taifa Jang’ombe zenye pointi sita kila moja lakini zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa. URA ipo katika nafasi ya nne na pointi nne, lakini kama itashinda mchezo dhidi ya Taifa inaweza kusonga mbele.

Katika mechi za awali, Simba ilizifunga Taifa Jang’ombe kwa mabao 2-1 na KVZ kwa bao 1-0 kabla ya kupata sare tasa na mabingwa watetezi wa mashindano hayo, URA.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema lengo lao ni kuhakikisha wanamaliza mechi za hatua ya makundi wakiongoza kundi lao, hivyo wanaupa uzito mkubwa mchezo wa leo na watahakikisha kuwa wanashinda.

“Mchezo wa mwisho hatukuweza kupata ushindi lakini hatukucheza vibaya, mchezo huu wa mwisho tutarekebisha makosa madogo yaliyojitokeza ili tuweze kushinda na kusonga mbele.

“Lengo letu ni kuongoza kundi, tunataka kumaliza kama vinara wa kundi na ili kufanikisha hilo ni lazima tujitahidi kushinda mchezo wa mwisho. Tuna timu nzuri na inaweza kutupatia kile tunachokihitaji.

“Sisi hatutazami tutakutana na nani huko mbele, hapana, tunatazama mchezo unaofuata. Jang’ombe Boys ni timu nzuri na tunapaswa kuipa heshima yake,” alisema Mayanja ambaye amewahi kuzifundisha Kagera Sugar na Coastal Union.

Kwa upande wake kocha wa Jang’ombe, Mund Seif King alisema Simba ni timu kubwa na wanaiheshimu katika mashindano hayO, lakini hilo haliwavunji moyo wa kupambana ili kuweza kupata pointi katika mchezo huo wa mwisho.

“Simba ni timu kubwa na imekuwa ikicheza vizuri katika mechi zao hapa, hivyo mchezo wetu wa mwisho utakuwa mgumu. Hata hivyo tutapambana, tulifanya vizuri hapa dhidi ya mabingwa watetezi, tunaweza kufanya hivyo dhidi ya Simba pia.

“Lengo letu ni kupata pointi mchezo wa mwisho na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali, ushindani ni mkubwa katika kundi letu,” alisema King ambaye ndiye kocha wa kwanza kuifundisha Azam FC inayomilikiwa na bilionea Said Salim Bakhresa.

Taifa Jang’ombe, URA kazi ipo

Mchezo wa usiku leo (Jumapili) utakuwa baina ya Taifa Jang’ombe na URA mchezo utakaoamua timu gani isonge mbele. Taifa wakishinda mchezo huo watakuwa wametinga moja kwa moja hatua ya nusu fainali wakati URA wakishinda watalazimika kutazama kwanza matokeo ya mechi ya kwanza kati ya Jang’ombe Boys na Simba.

Taifa wana pointi sita hivyo wakishinda watafikisha pointi tisa ambazo zinaweza kufikiwa na Simba pekee wakati URA ina pointi saba, hivyo ikishinda itafikisha pointi saba ambazo zinaweza kufikiwa na Simba na Jang’ombe Boys.