Simba wawachezea Gendarmarie picha kali

Muktasari:

  • Miamba hiyo ya Tanzania inaingia katika mchezo huo ikiwa na faida ya kushinda mabao mengi katika mchezo wa kwanza

 Simba itacheza na Gendarmarie kesho, Jumanne nchini Djibouti na wameandaa mbinu mbinu mbili kabambe za kuwamaliza.

Mbinu zilizoandaliwa na Wekundu hao wa Msimbazi ya kwanza ni kusoma mchezo ambapo watacheza kwa kujilinda na baada ya hapo ndipo watafunguka na kushambulia.

Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djumba amesema, katika dakika za mwanzoni watawaangalia kwanza wapinzani wao wanacheza vipi na baada ya hapo, ndiyo watafungua.

"Tutawaacha kwanza wacheze kwa kuwaangalia wana mbinu gani na tukishawasoma baada ya hapo, tutafungua na kuwashambulia,"alisema Djuma.

"Tunaongoza na mabao manne kikubwa ni kuyalinda na kuongeza mengine na kwa sababu kila kitu kinakwenda vizuri ninachokiamini, tutafanya vizuri tu katika mchezo huo."

Simba na Gendarmarie watacheza mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo katika mchezo wao wa awali wa Dar es Salaam, vijana hao wa Msimbazi walishinda mabao 4-0.