Simba yapania kuichakaza Gendarmarie

Muktasari:

Simba inahitaji sare tu au kufungwa chini ya mabao 3 ili kusonga mbele kwa mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho Afrika

Djibout.Timu ya Simba imeweka hadharani mbinu itakayotumia kuwang’oa wapinzani wao Gendarmarie katika mchezo wa leo saa 10: 00 jioni nchini Djibouti.

Simba na Gendarmarie zinatarajiwa kupepetana katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika. Mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wekundu wa msimbazi walishinda mabao 4-0.

Akizungumza mjini hapa jana, kocha msaidizi wa Simba Masoud Djuma alisema mbinu wanayotarajia kutumia ni kusoma mchezo huku wakicheza kwa kujilinda kabla ya kufunguka na kuanza kushambulia kwa nguvu.

Djuma alisema dakika za mwanzo watacheza kwa kuangalia kasi ya wapinzani wao kabla ya kujipanga na kuanza kusukuma mashambulizi langoni mwao.

"Tutawaacha wacheze kwa kuangalia wana mbinu gani wanatumia, tukishawasoma baada ya hapo tutafungua na kuwashambulia.

"Tunaongoza mabao manne kikubwa ni kulinda na kuongeza mengine kwasababu kila kitu kinakwenda vizuri ninachokiamini, tutafanya vizuri katika mchezo huo,”alisema Djuma raia wa Burundi.

Simba inapewa nafasi ya kusonga mbele katika mchezo wa raundi ya kwanza kutokana na mtaji mzuri wa mabao na huenda ikavaana na Al Masry ya Misri.