Simba yaanza kutekeleza agizo la JPM

Muktasari:

  • Rais Magufuli aliitaka klabu ya Simba kuleta kombe la Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dar es Salaam. Klabu ya Simba imeanza kutekeleza agizo la Rais John Magufuli, alilotoa kwa viongozi wa klabu hiyo akiwataka kutwaa ubingwa wa Afrika.

Rais Magufuli aliitaka klabu ya Simba kuleta kombe la Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba imekata tiketi kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na inatarajiwa kukutana uso kwa uso na miamba inayotamba katika medani ya soka.

Baada ya kuchafua rekodi ya kutofungwa baada ya juzi kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar, Rais Magufuli aliitaka klabu hiyo kujiandaa kikamilifu kwa mashindano ya kimataifa.

Rais Magufuli alisema hakuridhishwa na kiwango cha Simba katika mchezo huo na aliitaka klabu hiyo kufanya maandalizi ya kutosha kama inataka kutwaa ubingwa wa Afrika.

Agizo la Rais Magufuli limeanza kuleta matokeo chanya kwa klabu hiyo ambayo jana ilianza kuweka mikakati ya kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo.

Wanachama wa Simba jana walipitisha rasmi mabadiliko ya katiba yatakayoifanya iendeshwe kwa mfumo wa kampuni ambayo itakuwa chini ya usimamizi wa wanachama na mwekezaji.

Pia vigogo wa klabu hiyo kongwe nchini walitangaza mikakati ya kuwa na timu bora itakayotamba katika mashindano mbalimbali yakiwemo ya kimataifa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema wana deni kwa Rais Magufuli na wameanza mkakati wa kulipa.

“Yule ni Rais wa nchi kauli yake ni amri kwetu sisi tunakwenda kujipanga kwa sababu kauli ndio imetoka jana (juzi). Tunakwenda kujipanga kuhakikisha tunatekeleza yale ambayo ametuelekeza.

“Japokuwa mpira haupo hivyo, lakini sisi tutahakikisha tunatengeneza mazingira ya kwenda huko ambako Rais anataka twende kwa sababu hata sisi tuna tamani kufika huko.

“Nimeahidi kwenye mkutano na wamenisikia tunakwenda kuhakikisha mwakani hatukamatiki na hatushikiki,” alisema Try Again.

Kigogo huyo alitoa ahadi hizo kwa wanachama wa Simba zaidi ya 900 waliohudhuria mkutano wa klabu hiyo uliofanyika jana Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam ambao walibariki klabu hiyo kujiendesha katika mfumo wa kampuni.

“Nawaambieni Wanasimba, baada ya mabadiliko haya Simba itakuwa na mafanikio makubwa ya ndani na nje ya uwanja.

“Tutahakikisha tunaimarisha kikosi chetu kwa kumsajili mchezaji yeyote mzuri tutakayemuhitaji kwa gharama yoyote ile ya fedha ambayo itahitajika.

“Na kuanzia msimu ujao tutaanza kutumia uwanja wetu kwenye mechi mbalimbali za timu yetu,” alisema Try Again.

Akitoa ufafanuzi wa vifungu vilivyopo kwenye Katiba mpya ya Simba, mwanasheria wa klabu hiyo, Wakili Evodius Mtawala alisema mwekezaji ambaye ni mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’, atamiliki asilimia 49 na wanachama asilimia 51.

“Kwa mujibu wa sheria ya nchi, chombo kinachotambulika kwa msajili wa vyama vya michezo ni baraza la wadhamini wao ndiyo watakuwa na jukumu la kusimamia hisa asilimia 51 na 49% zitakuwa za mwekezaji.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini atakuwa na nafasi ya kuingia kwenye bodi na atakuwa na asilimia moja,” alifafanua Wakili Mtawala.

Wakili Mtawala alitumia zaidi ya dakika 45 kuwafafanulia wanachama wa Simba namna mfumo huo utakavyoendesha klabu yao yenye maskani Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.

Hata hivyo, hakuna mwanachama aliyepinga hatua hiyo na kila mmoja aliridhia mabadiliko hayo.

Hatua hiyo imekata kiu ya mmoja wa wazee wa Baraza la Wadhamini chini ya mwenyekiti wake, Hamisi Kilomoni ambaye alikuwa akitaka mabadiliko lakini kwa asilimia ambazo ndizo wamekubaliana kwa sasa.

Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema kauli ya Rais Magufuli ni agizo ambalo ni lazima litekelezwe.

“Jana (juzi) Mheshimiwa Rais alisema anataka kuiona Simba inatwaa ubingwa wa Afrika, hili ni agizo na sisi kwenye wizara tunaanza kulisimamia.

Kinachohitajika ni ubingwa wa Afrika na siyo historia. Rais anafahamu kwamba Simba ina historia kubwa lakini yeye anachotaka ni ubingwa wa Afrika tu,” alisema Waziri Mwakyembe.

Wakati huo huo, Kaimu Rais wa Simba alimkabidhi Dk Mwakyembe jezi namba 19 kwa niaba ya Rais Magufuli.