Simba yainyima raha Lipuli

Muktasari:

  •  Amri anasema kwa  namna Simba ilivyo sasa si ya kuwekeza nguvu kwa Emmanuel  Okwi na John Bocco pekee bali ni kuwatazama wachezaji wote wa kati ambao wana uwezo mkubwa wa kufunga. 

BENCHI la ufundi la Lipuli limekiangalia kikosi cha Simba watakaocheza nao keshokutwa Jumamosi kwa umakini na kusisitiza wata 'dili' na safu zao mbili ambazo wanaona ndiyo zitawasumbua ambazo ni kiungo na ushambuliaji.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Amri Said amesema, Simba ya sasa ni hatari kutokana na jinsi wanavyopambana kwa ajili ya ubingwa ambao waliukosa kwa takribani miaka mitano, jambo linalowafanya wajihami mapema .

"Hatuwezi kujiongepea na kuona Simba kwetu si lolote, wakati tunawasikia wenzetu wanatembezewa kipigo, lazima tuangalie maeneo ambayo yatakuwa mwiba kwetu ndio tuyafanyie kazi kikamilifu kama safu ya kiungo na ushambuliaji," anasema Amri ambaye ni kocha na mchezaji wa zamani wa Simba.

Anasema kwa  namna Simba ilivyo sasa si ya kuwekeza nguvu kwa Emmanuel  Okwi na John Bocco pekee bali ni kuwatazama wachezaji wote wa kati ambao wana uwezo mkubwa wa kufunga.

"Ukisema uwe makini na Bocco na Okwi, yupo mtu kama Shiza Kichuya anaibuka tu unashangaa kafunga, yupo Shomary Kapombe licha ya kwamba ni beki lakini ana mashambulizi makali kutoka pembeni, tupo kamili kuhakikisha hatufanyi makosa kama si pointi tatu, lazima tugawane moja moja," anasema.