Simba yapaa Djibouti kwa tahadhari

Muktasari:

  • Kikosi cha Simba jana kiliondoka kwa mafungu kwenda Djibouti kurudiana na Gendarmaria katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa kesho.

Timu ya Simba, imepanga kucheza kufa au kupona katika mchezo wa marudiano dhidi ya vibonde Gendarmerie Nationale FC ya Djibouti.

Kikosi cha Simba jana kiliondoka kwa mafungu kwenda Djibouti kurudiana na Gendarmaria katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa kesho.

Kocha wa Simba Masoud Djuma alisema kuwa wanakwenda Djibouti kuanza upya katika mchezo huo wa maruduano.

“Mpira umebadilika, hutakiwi kuwa na dhana ya uwepo wa timu dhaifu na ngumu. Tunataka kuvuka hatua hii, ushindi unaweza kuwa na faida zaidi kwetu, mchezo uliopita umepita kilichopo ni kutafuta matokeo mengine mapya,” alisema kocha huyo msaidizi muda mfupi kabla ya kupanda ndege.

Simba iliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam saa 8:57 mchana na wachezaji 20, viongozi saba na mashabiki wachache.

Kundi la kwanza liliondoka saa 11:30 na jingine likiwa na wachezaji Yusuph Mlipili, Juuko Murshid, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude liliondoka saa 12:40 jioni.

Endapo Simba itavuka hatua ya awali ina nafasi kubwa ya kukutana na Al Masry ya Misri katika mchezo wa raundi ya kwanza.

Nahodha wa timu ya Simba, John Bocco, aliyeumia katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mwadui, alisema watahakikisha wanapata ushindi.

“Mazingira ya ugenini yanaweza kubadili sura nzima ya mchezo, lakini pamoja na yote hayo tunataka kusonga mbele tutacheza kwa nguvu zetu zote,” alisema Bocco.

Awali, mshambuliaji huyo alihusishwa kutokwenda Djibouti baada ya kushindwa kufanya mazoezi siku ya mwisho, lakini jana aligoma kuzungumzia afya yake.

Kiungo Mghana James Kotei alisema watazingatia mafunzo waliyopewa na benchi la ufundi ili kupata pointi tatu katika mchezo huo.

“Kushinda ugenini sio kazi nyepesi lakini tuna lengo la kushinda mchezo wa marudiano, tunategemea upinzani mkali kwa sababu watakuwa nyumbani kwao,” alisema Kotei.

Naye Shiza Kichuya alisema itakuwa aibu kwa Simba endapo itafungwa na kutupwa nje katika Kombe la Shirikisho Afrika.