Singida United yaipiga bao Yanga

Muktasari:

  • Singida United imesajili wachezaji saba wapya tangu kumalizika kwa msimu  wa Ligi Kuu

Arusha. Mshambuliaji Eliuter Mpepo amesaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia Singida United akitokea Tanzania Prison.

Mpepo ametua singida wakati kukiwa na tetesi za kusakwa na Yanga FC, lakini ameamua kuwafuata walima alizeti hao watakaokuwa chini ya kocha mkuu Hemed Morocco baada ya kuachana na Mholanzi Hans van der Pluijm aliyehamia Azam FC.

Aidha  Mpepo anakuwa mchezaji wa saba kusajiliwa Singida United kuelekea msimu ujao, wengine ni Daniel Lyanga kutoka Fanja ya Oman, Tibar John kutoka Ndanda FC, Habib Kiyombo kutoka Mbao FC, Mbrazil Felipe Oliveira na Muivory Coast, Diaby Amara.

Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga pamoja na kumtambulisha mchezaji huyo, alisema wana matumaini makubwa na mchezaji huyo hasa baada ya kuona kiwango chake katika mechi walizocheza na Prison msimu uliopita.

“Mpepo anazimudu vyema nafasi zote za ushambuliaji na amesajiliwa kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na prison,” amesema.

Mpepo anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa Singida United kutoka Tanzania Prisons, baada ya kiungo Kazungu Mashauri aliyesajiliwa mwezi uliopita.

“Kwa timu iko mapumzikoni na muda wowote wiki ijayo watarudi kuanza kambi hapo tutawatambulisha wachezaji wote ambao watawakilisha Singida kufanya makubwa zaidi ya msimu huu,” alisema Sanga.