Singida United kucheza Kagame kibabe!

Dar es Salaam. Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki (Cecafa)  limethibitisha  nafasi za  Yanga kuwa itachukuliwa na Singida United kwenye Kombe la Kagame ambalo litaanza kutimua vumbi nchini  Juni 29, hadi  Julai 13.

Yanga  ilitangaza kujitoa kwenye michuano hiyo maarufu ukanda wa Afrika Mashariki na Kati  kwa lengo la kupumzisha kikosi chao kabla ya kuendelea na michezo ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika, Julai 18 ambapo wao watakipiga na Gor Mahia ya Kenya ugenini.

Mbali na Yanga klabu ya St. George ya nchini Ethiopia pia walijitoa na baraza hilo likaipa nafasi klabu ya APR ya Rwanda ili kuziba nafasi yao.

Klabu zitakazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na Simba, Azam FC pamoja na Singida United za Tanzania Bara, JKU ya Zanzibar na Rayon Sports ya Rwanda.

Nyingine ni Dakadaka ya Somalia, Ports ya Djibouti, Lydia Ludic ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya, St. George ya Ethiopia, Kator FC ya Sudan Kusini na Vipers SC ya Uganda.

Cecafa pia imethibitisha  Kombe la Chalenji kwa wanawake litafanyika nchini Rwanda kuanzia Julai  19 hadi 29 mwaka huu.

Mataifa yanayo tarajiwa kushiriki ni  Rwanda, Kenya, Uganda, Tanzania, Djibouti, Zanzibar na  Ethiopia.