Singida United ajitoa Ligi Kuu akili Kombe la FA

Muktasari:

  • Bingwa wa Kombe la FA anapata tiketi ya moja kwa moja kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika

Mwanza. Mshindwe wenyewe, ndivyo unavyoweza kusema kwani Mabosi wa Singida United wamesema kuwa suala la ubingwa wa Ligi Kuu sasa wameziachia Simba na Yanga, huku wao wakielekeza nguvu zao Kombe la FA.

Timu hiyo ambayo imefanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano hayo, inatarajia kujitupa uwanjani kesho, Jumamosi kuwakabili JKT Tanzania, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Mkurugenzi wa Klabu hiyo, Clement Sanga alisema kuwa kwa sasa mbio za kutwaa taji la Ligi Kuu wamewaachia Simba na Yanga, huku wao wakikomalia ubingwa wa Kombe la FA.

Sanga alisema kuwa katika kuhakikisha wanatwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza, wameamua mchezo huo mashabiki wote mkoani Singida wataingia bure uwanjani kushuhudia mtanange huo.

Kigogo huyo aliongeza ili kuhakikisha wanafika fainali na kutwaa ubingwa, wameamua kuwapa hamasa nyota wao, ambapo kila bao watakalofunga,watalinunua kwa Sh1 milioni.

Alisema kuwa malengo yao kwenye mashindano hayo kutwaa taji ili kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

“Tumejipanga vizuri na tayari kuna wadau ambao wametoa hamasa kwenye mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya JKT, bao moja litalipwa kwa Sh1 milioni,” alisema Sanga.